Aliyekuwa kiongozi mkuu wa chama cha ACT WAZALENDO, Zitto Kabwe amevitaka vyama vyote vya siasa nchini kuendana na mahitaji na muelekeo wa Taifa pindi vinapotengeneza ilani za uchaguzi.
Akichangia kama mmoja wa jopo la watoa mada wakuu kwenye Kongamano la Kwanza la Kitaifa kuhusu Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Zitto alionya juu ya mpishano kati ya uelekeo wa Taifa na mipango ya vyama vya siasa.
Ili kuondoa mkanganyiko wa sera na utekelezaji wa miradi ya kimaendeleo, Mh. Zitto Kabwe ametoa rai kwa vyama vyote nchini kuitumia Dira ya Taifa ya Maendeleo kama nguzo kuu ya kuwaelekeza mahitaji, kiu na shauku ya wananchi ambao ndio wapiga kura.
Katika mchango wake juu ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, Mh. Zitto alitumia fursa hiyo kusisitiza juu ya mijadala chanya ya ana kwa ana inayoshirikisha wadau wa sekta mbalimbali kwenye jamii yenye azma ya ufuatiliaji wa kina wa hatua kwa hatua utekelezaji wa kinachokubaliwa kwa pamoja kwenye dira hiyo.