Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetumia kiasi cha shilingi bilioni 5.4 kugharamia ununuzi wa vifaa na vifaa tiba kwa ajili ya jengo la huduma za Mama na Mtoto katika Hospitali ya Kanda Mbeya.
Uwekezaji huo mkubwa na wa kipekee kuwahi kufanywa na Serikali mkoani humo, umeangazia kuwasogezea karibu wananchi, huduma bora na za kibingwa, ambao hapo awali wengi walikuwa wanalazimika kusafiri hadi Jijini Dar es salaam kufuata huduma bora.
Kupitia majibu ya swali la msingi, lililoelekezwa wizara ya afya na mbunge wa viti maalum Mh. Suma Ikenda Fyandomo, Naibu Waziri wa Afya Mh. Dkt. Godwin Mollel, alieleza kuwa kupitia maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, fedha hizo zilishaidhinishwa.
Akifafanua zaidi, Naibu Waziri Mollel aliliambia bunge kuwa manunuzi ya vifaa vilivyokusudiwa yalishafanyika na kukamilika pamoja na zoezi la ufungaji wa vifaa hivyo. Naibu Waziri Mollel alieleza kupitia majibu yake kuwa tayari huduma za kibingwa zimeshaanza kutolewa hispitalini hapo kwa akina mama na watoto.