728 x 90

Wazalishaji wa mafuta waipongeza serikali ya Rais Samia kuondoa VAT.

  • June 25, 2024
Wazalishaji wa mafuta waipongeza serikali ya Rais Samia kuondoa VAT.

Katika hali ya kuonyesha kuridhishwa na uwezeshaji unaofanywa na Serikali ya awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Chama cha wasindikaji wa mafuta ya kula ya alizeti Tanzania (TASUPA), kimesema kitendo cha Serikali kuondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwa wazalishaji wa ndani, itachochea ongezeko la ulimaji wa alizeti na uwekezaji mkubwa zaidi wa viwanda vya kuongeza thamani.

Hatua nyingine ya Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyopongezwa na chama hicho ni ya kutoa mapendekezo ya kuanza kutoza ushuru wa forodha kwa mafuta ya kula yanayoagizwa kutoka nje.

Hatua hii imetajwa na chama hicho kama nyenzo muhimu ya kuvilinda viwanda vya ndani, na kuwahamasisha wazawa wengi zaidi kushiriki katika uwekezaji utakaosaidia kuinua uchumi wa nchi.

Pongezi hizo zimetolewa na mwenyekiti wa chama hicho Ndg. Ringo Iringo ambae pia alidokeza juu ya ukuaji wa sekta ya mafuta ya kula nchini ambayo amekiri kuwa imekuwa kwa kasi katika kipindi cha miaka mitatu kutokana na mazingira wezeshi na rafiki yaliyoratibiwa na Serikali ya awamu ya Sita, chini ya usimamizi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumzia mchango wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa sekta hiyo changa, Ndg. Ringo amebainisha kuwa Rais Samia amewezesha urahisi wa upatikanaji wa mashine na vipuri vinavyotumika kukamua alizeti na kusafisha mafuta ili kuyapa thamani zaidi sokoni kwa kuyawezesha kushindana kwa ubora na yale yanayotoka nje ya nchi.

Katika mkutano huo wa chama hicho na waandishi wa habari, mwenyekiti huyo Ndg. Ringo aliipongeza Serikali kwa kutoa mapendekezo katika bajeti yake ya mwaka 2024/25 ya kuanza kutoza ushuru wa forodha kwa mafuta ya kula yanayoingizwa nchini kwa asilimia 25 au 35 au dola za marekani 250 kwa tani moja kwa mafuta ghafi au dola za marekani 500 kwa tani moja kwa mafuta yaliyosafishwa.

Akigusia pia hali ya viwanda vya mafuta ya kula nchini, ndg. Ringo aliwaambia waandishi hao kuwa, wazalishaji wa mafuta ya kula wa umoja huo wana uwezo wa kuzalisha jumla ya tani za ujazo 5000 kwa siku, hali ambayo inawalazimu kuwa na uhakika wa kupata walau tani za ujazo wa 1,800,000 kwa mwaka za alizeti.

Kupitia maelezo yake, Mwenyekiti Ringo aliongezea kuwa kutokana na kuimarika kwa mazingira ya uendeshaji wa shughuli zao, wanatarajia kuwa ifikapo mwaka 2027, hakutakuwa na changamoto ya upatikanaji wa mafuta ya kula nchini, na wao kama TASUPA wanatarajia kuwa watakuwa wameshaanza kuuza mafuta ya kula nje ya nchi, hususan nchi za Jamhuri ya Kidemikrasia ya Congo na Comoro ambazo zina fursa kubwa ya soko la mafuta ya kula.