728 x 90

Vilabu vya Ligi Kuu vibadili mitazamo juu ya makocha.

  • June 5, 2024
Vilabu vya Ligi Kuu vibadili mitazamo juu ya makocha.

Ukijivika mabomu, usiogope kulipuka. Ni sawa na machalii wa Arusha wanavyotusisitiza tusiwe na moja kwenye mbili!! Ukishaamua kufanya uamuzi, kaa nao. Uwe mzuri au mbaya ishi nao.

Kufikia nusu ya msimu ulioisha, klabu kadhaa za Ligi Kuu ya Tanzania NBC zilichukua maamuzi ya kubadili sura kwenye mabenchi yao ya ufundi. Kwa bahati mbaya huwa hatuwekewi hadharani taswira kamili ya kufurushwa kwa makocha kutoka kwenye timu zetu. Sanasana tunaonyeshwa wakishukuriwa kwa “Thank You” na kutakiwa kila la kheri huko waendako.

Najiuliza sana kama viongozi wa vilabu vyetu huwa tayari kutokuwaingilia makocha katika majukumu yao. Ni kidonda kisichoelekea kupata tiba muda wowote wa karibuni. Bado ligi zetu zinakumbwa na hadithi nyingi za chini ya kapeti kuhusu makocha kupangiwa vikosi na matumizi makubwa ya vimemo kuhusu wachezaji wapi wacheze na wapi wasipewe kipaumbele.

Kwa jinsi hii, kunakuwa hakuna ulazima wa kuwa na walimu kwenye hizi timu. Ukosefu wa mipaka ya kimajukumu ni ugonjwa hatari unaozuia kukua kwa aina yeyote iwayo ile kwa hiki kiwanda cha soka.

Kama ilivyoandikwa kwenye vitabu vya dini kuwa ya kaisari tumpe kaisari, basi na ya makocha tuwaachie makocha. Tusiwaingilie kwenye kazi zao na kuwapandikizia mawazo au falsafa au mbinu wasizozitaka. Tuwape uhuru wa kutumia kikamilifu maarifa yao na kujitolea kwa nguvu zao zote. Pale tu tunapomnyima Kaisari kilicho chake, hali haitendelea kuwa shwari. Pale tu tunapoanza kumpangia mwalimu, huyu acheze na yule asicheze tunakuwa tumemnyima uhuru na kumuwekea vikwazo vya kutupa alichokusudia.

Kama mbwembwe zilivyo kubwa wakati wa kuwatambulisha wakufunzi wapya, basi vivyo hivyo na utayari wetu wa kuwaachia mamlaka ya kuwa na maamuzi kamili juu ya mbinu, vikosi, nidhamu na usajili unatakiwa kuwa juu.

Inakuwa ni ngumu kumdai mwalimu kama hahusiki moja kwa moja kuamua hatma ya timu kiuchezaji na kupitia hiyo matokeo ya timu. Tutakuwa tunafanya mchezo huo huo wa kuleta sura mpya kila siku na kuendelea na ujinga wa kuingilia majukumu ya watu huku tukitegemea matokeo tofauti.

Hii ni tabia isiyofaa wala isiyopendeza. Inaharibu picha ya ligi yetu na kueneza sifa mbaya kupitia kumbukumbu wanazobaki nazo makocha wanaoingiliwa kwenye majukumu yao. Ya kaisari tumpe tu. Tuwaache makocha wafundishe na viongozi mzisimamie timu zenu kwa kuzitengenezea mazingira mazuri ya kutoa ushindani wenye hadhi na weledi.