Kupitia juhudi za Serikali ya awamu ya Sita za kuendeleza sekta ya kilimo, Tanzania imepata mafanikio makubwa katika utekelezaji wa mpango wa maendeleo wa taifa.
Mafanikio haya yametokana na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, ambaye ameweka msukumo mkubwa katika uwekezaji wa rasilimali fedha na kuinua uwezo wa watu wanaohudumia na kusimamia sekta hiyo.
Kulingana na taarifa ya hali ya uchumi kwa mwaka 2023 na mpango wa maendeleo wa taifa wa mwaka 2024/25, kumekuwa na ongezeko la uzalishaji wa mazao ya kilimo kutoka tani 30,569,893.52 mwaka 2020/21 hadi tani 36,409,694.83 mwaka 2022/23.
Ongezeko hili limejumuisha pia uzalishaji wa mazao ya nafaka, ambapo uzalishaji umepanda kutoka tani 9,046,377.10 mwaka 2020/21 hadi tani 11,420,327.06 mwaka 2022/23.
Ongezeko hili limeimarisha usalama wa chakula nchini, na kufikia asilimia 124 ya utoshelevu wa chakula mwaka 2022/23, likikaribia lengo la asilimia 130 ifikapo mwaka 2025/26.
Matokeo haya chanya yanayoliweka taifa katika hali ya utulivu kwa uhakika wa chakula, yanatambulika kama mchango mkubwa wa Rais Samia Suluhu Hassan.
Kwa kuongezeka kwa uzalishaji wa mazao ya kilimo na nafaka, ripoti inaonyesha kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la mauzo ya bidhaa za Tanzania nje ya nchi, ikiwemo bidhaa za kilimo.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaendelea kuipa sekta ya kilimo kipaumbele kwa kuendeleza utekelezaji wa sera za mageuzi zinazosukuma ukuaji wa sekta ya kilimo kulingana na mabadiliko ya teknolojia duniani na mahitaji ya soko la kimataifa.