728 x 90

Ujenzi wa Barabara ya Mwendokasi Awamu ya Nne Unaendelea Vizuri.

  • July 25, 2024
Ujenzi wa Barabara ya Mwendokasi Awamu ya Nne Unaendelea Vizuri.

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa Serikali kupitia Wakala ya Barabara (TANROADS) inaendelea na ujenzi wa miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam Awamu ya Nne (BRT 4) kuanzia Daraja la Kijazi (Sam Nujoma) – Mwenge – Maktaba ya Taifa (Posta) yenye urefu wa kilometa 13.5.

Pia, ujenzi wa miundombinu ya Mabasi hayo unaendelea kuanzia Mwenge – Tegeta (DAWASA) yenye urefu wa kilometa 15.63 ambapo ujenzi huo unatekelezwa na Wakandarasi wawili M/s China Geo Engineering na M/s Shandog Group Co. Ltd.

Bashungwa ameeleza hayo Mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na wakazi wa Mkoa huo ambapo pamoja na mambo mengine amesema Serikali imejipanga vyema kuufungua Mkoa huo kwa miundonbinu ya uhakika ili kutatua kero za foleni za magari.

“Tunao Wakandarasi wanaojenga barabara ya Mwendokasi kuanzia Serena Hoteli kuelekea Mwenge na kutoka Mwenge kuelekea Ubungo (Daraja ya Kijazi), Wakandarasi wako kazini na fedha ipo”, amesema Bashungwa.

Bashungwa amemtaka Mkandarasi Sinohydro Corporation anayetekeleza ujenzi wa Miundombinu ya Mabasi Yaendayo Haraka Awamu ya Tatu (BRT 3) katika barabara ya Tanganyika Motors – DIT, Uhuru (Buguruni – Msimbazi) Bibi Titi na Shaurimoyo (Karume – Bohari), kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha mradi huo kwa wakati kulingana na mkataba.

Aidha, Waziri Bashungwa amefafanua kuwa TANROADS wapo katika hatua ya manunuzi ya kumpata Mkandarasi atakayejenga Daraja la Mzinga na kufanya upanuzi wa barabara kuanzia Mbagala Rangi Tatu hadi Vikindu ili kupunguza foleni ya magari na kuondoa adha ya watumiaji wa barabara hiyo kwa wananchi wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.

Amefafanua kuwa katika Bajeti ya 2024/25, Serikali imejipanga kufanya upanuzi wa njia nne barabara ya Mwaikibaki (Morocco – Africana) yenye urefu wa kilometa 11.7, itakayoanzia Morocco kuelekea Africana kupitia Kawe ya Chini, Kawe – Lugalo pamoja na kipande cha Mwalimu Nyerere cha kwenda Rose Garden.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila ameiomba Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi kuingia Ubia na Sekta Binafsi kwa ajili ya ujenzi wa barabara na madaraja ya kulipia tozo kama ilivyokuwa katika Daraja la Nyerere Mkoani Dar es Salaam ili fedha hizo zinazopatikana ziweze kutumika katika ujenzi na matengenezo ya miundombinu ya barabara na madaraja iliyoharibika.
Share this: