Shirika la Madini la Taifa (STAMICO), kupitia kampuni tanzu ya STAMIGOLD, limewasilisha mpango wa uwekezaji wa kampuni hiyo kuhusu uendelezaji wa miradi ya madini kwa Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, jijini Dodoma.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Deusdedith Magala, amesema kuwa tangu kuanza uzalishaji hadi Machi 2024, mgodi umezalisha na kuuza jumla ya wakia 122,964.53 za madini ya dhahabu na wakia 16,662.54 za madini ya fedha.
Magala ameongeza kuwa mgodi umeendelea na uhakiki na utafiti kupitia njia mbalimbali za ukusanyaji wa taarifa na ukadiriaji upya wa akiba ya mashapo ya mgodi. Hadi Aprili 2024, mgodi ulikuwa na akiba ya mashapo ya wakia za dhahabu 114,190 ambazo zitachimbwa kwa miaka mitano.
Wajibu wa STAMIGOLD kwa Jamii
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge Nishati na Madini, Mathayo David Mathayo, ameitaka wizara kuisimamia na kufuatilia kwa karibu kampuni ya STAMIGOLD ili iwe kampuni yenye manufaa kwa taifa.
Naibu Waziri wa Madini, Dkt. Steven Kiruswa, amezungumzia wajibu wa mgodi kwa jamii (CSR), akieleza kuwa wizara imepokea maoni yaliyowasilishwa na kamati kuhusu mapitio ya kanuni za CSR na imeanza kuyafanyia kazi ili kuziboresha inapohitajika.
Malengo ya Wizara ya Madini
Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini, Kheri Mahimbali, amesema malengo ya wizara ni kuipeleka mbali STAMIGOLD ili iwe mgodi mkubwa utakao tambaa sehemu mbalimbali ndani ya nchi pamoja na kutambulika na taasisi kubwa za fedha.
STAMICO ilianzishwa rasmi mwaka 1972 kwa lengo la kuwekeza kimkakati katika miradi ya madini na uvunaji wa rasilimali madini ndani ya mnyororo mzima wa sekta ya madini.