728 x 90

Tsh Bil. 16 kujenga shule za sayansi za wasichana kila mkoa nchini.

  • June 12, 2024
Tsh Bil. 16 kujenga shule za sayansi za wasichana kila mkoa nchini.

Naibu Waziri Ofisi ya Rais – TAMISEMI anayeshughulikia Elimu, Mhe. Zainab Katimba, amesema kabla ya kukamilika kwa mwaka wa fedha 2023/24, Serikali imetoa kiasi cha shilingi bilioni moja kwa kila shule mpya 16 za bweni za wasichana zilizojengwa ili kukamilisha miundombinu iliyosalia.

Fedha za Kukamilisha Miundombinu
Mhe. Katimba alitoa taarifa hiyo bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha maswali na majibu wakati akijibu swali la nyongeza la Mhe. Emmanuel Lekishon Shangai, Mbunge wa Jimbo la Ngorongoro, aliyetaka kujua ni lini Serikali itapeleka fedha kwa ajili ya kujenga uzio na nyumba za watumishi katika shule hizo ambazo kwa sasa ujenzi wake umefikia asilimia 85.

“Serikali imepeleka bilioni moja katika shule zote 16 za wasichana ambazo zilipelekewa bilioni tatu kwa awamu ya kwanza kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya msingi ikiwemo vyumba vya madarasa 10, chumba cha TEHAMA kimoja, maktaba moja, nyumba za walimu tatu, na mabweni manne. Serikali itapeleka fedha hiyo kwa ajili ya kukamilisha miundombinu ili shule zetu hizi ziweze kuwa zimekamilika na wanafunzi waweze kuingia na kuanza masomo yao,” alisema Mhe. Katimba.

Ujenzi wa Shule za Wasichana Arusha
Awali, akijibu swali la msingi la Mhe. Zaytun Seif Swai, Mbunge wa Viti Maalum, aliyetaka kufahamu ni lini Serikali itaanza kujenga shule ya Wasichana Arusha ambayo ilipangwa kujengwa katika Wilaya ya Longido, Kata ya Enkikret, Mhe. Katimba alisema, “Serikali kupitia Mradi wa Kuboresha Elimu ya Sekondari imepanga kujenga shule 26 za bweni za wasichana za kitaifa katika mikoa yote nchini. Lengo la shule hizi ni kuongeza fursa kwa wanafunzi wa kike kusoma masomo ya sayansi na kuwaepusha na vishawishi vinavyosababisha kukatisha masomo.”

Awamu Mbili za Ujenzi
Mhe. Katimba aliongeza kuwa ujenzi wa shule hizi umefanyika katika mikoa yote kwa awamu mbili, ambapo awamu ya kwanza ilianza kwa mikoa ya Kagera, Shinyanga, Mwanza, Singida, Pwani, Songwe, Lindi, Dar es Salaam, Njombe na Ruvuma. Awamu ya pili imefanyika katika mikoa iliyobaki, ikiwemo Mkoa wa Arusha ambapo ujenzi unafanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Longido na umefikia asilimia 85.