Serikali ya awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kujenga reli ya mwendokasi ya Mtwara hadi Mbamba bay.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi Mh. David Kihenzile bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akijibu swali la mbunge wa viti maalum Mh. Jacqueline Msongezi lililokuwa linataka kujua ni lini Serikali itaanza reli ya mwendokasi ya Mtwara-Mbamba bay.
Mh. Kihenzile aliliambia bunge kuwa, Serikali kupitia shirika la Reli Tanzania (TRC) limekamilisha upembuzi na usanifu wa awali kwa ajili ya ujenzi wa njia ya reli ya Mtwara hadi Mbamba bay na matawi yake ya Liganga na Mchuchuma yenye urefu wa kilomita 1000.
Akiendelea na majibu yake, Naibu Waziri Mh. Kihenzile amelitaarifu bunge kuwa, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejikita katika kutafuta rasilimali fedha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huu kwa utaratibu wa ubia baina ya sekta ya umma na binafsi. Naibu Waziri Kihenzile ameitaja hatua ya awali kuchukuliwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/25 ni kutenga kiasi cha shilingi 702,625,000 kwa ajili ya kumuajiri mshauri muelekezi atakaekuwa na jukumu na kuandaa andiko na makabrasha ya zabuni yatakayosaidia kumpata mzabuni mwekezaji kwa utaratibu wa ubia kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP).
Akimalizia kujibu swali hilo, Naibu Waziri David Kihenzile amewaomba wananchi wa Liwale kuendelea kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan na kuendelea kuwa na subira wakati Serikali inaendelea kukamilisha maandalizi ya kuanza ujenzi wa njia hiyo kwa kiwango cha standard gauge.