Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuhakikisha inafikisha huduma za afya kwa wananchi wake wa mijini na vijijini.
Akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Mtwara Vijijini, Mh. Shamsia Azizi Mtamba, aliyetaka kujua ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa kituo cha afya mkunwa- Mtwara vijijini, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Mh. Zainab Katimba ameliambia bunge kuwa, kituo cha afya cha Mkunwa kilianza mwaka 2019/20 ambapo ujenzi wake ulianza kwa ramani ya majengo ya hospitali.
Kupitia majibu yake ya Serikali kwa Bunge, Naibu Waziri Mh. Katimba aliliambia Bunge kuwa jumla ya shilingi bilioni 1.5 zimeshatolewa kwa ajili ua ujenzi wa majengo saba (7), ambayo ni jengo la OPD, jengo la wazazi, jengo la dawa, jengo la maabara, jengo la mionzi, nyumba ya mtumishi na kuchomea taka.
Akielezea hatua yaliyofikia majengo hayo, Naibu Waziri huyo wa TAMISEMI, ameliambia bunge kuwa majengo hayo yapo kwenye hatua mbalimbali za ujenzi na ili kukamilika, kiasi cha shilingi milioni 900 kinahitajika.
Naibu Waziri Mh. Katimba amelihakikishia bunge kuwa, Serikali ya awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, inaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya ukamilishaji wa majengo hayo.