Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha viwanda vya kuchinja, kuchana na kusindika mifugo, vyenye ubora wa kimataifa vinajengwa nchini.
Maelezo hayo yametolewa na Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Alexander P. Mnyeti bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la mbunge wa jimbo la Mpendae, Mh. Toufiq Salim Turky aliyetaka kufahamu, Serikali ina mpango gan kuhakikisha viwanda vya kuchinja, kuchana na kusindika mifugo vinavyokidhi vigezo vya kusafirisha nje ya nchi vinajengwa nchini.
Kupitia majibu ya swali hilo, Naibu Waziri, Mh. Mnyeti alilieleza bunge kuwa, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za makusudi katika kuweka mazingira wezeshi ili kuvutia sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuchinja, kuchakata na kusindika mifugo na mazao yake vinavyokidhi vigezo shindani vya kusafirisha nje ya nchi.
Aidha, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mh. Mnyeti alizitaja mbele ya bunge baadhi ya hatua ambao zimekuwa zikichukuliwa na Serikali, ikiwa ni pamoja na kuhamasisha uanzishaji wa viwanda kupitia eneo maalum la uwekezaji (EPZ) kwa ajili ya soko la nje ya nchi, ambapo wawekezaji hupata msamaha wa kodi ya mapato, kodi ya mitambo na vifaa vya kuchakata na kusindika nyama. Mh. Mnyeti amesema pia kuwa, Serikali imeondoa kodi ya ongezeko la thamani (VAT) kwenye vifaa vya kuchakata nyama kwa wadau wanao omba msamaha huo.
Naibu Waziri, Mh. Mnyeti amelifahamisha bunge kuwa kutokana na jitihada hizi za Serikali, viwanda vyenye viwango na ithibati ya kimataifa ya kusafirisha nyama nje ya nchi vimeongezeka kutoka viwanda viwili (2) vilivyokuwepo mwaka 2018/19 hadi kufikia viwanda sita (6) mwaka 2023/24.