Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imedhamiria kukamilisha mradi wa maji ya Ziwa Victoria kutoka Butiama kwenda Nyamuswa – Bunda.
Naibu Waziri wa Maji, Mh. Mhandisi Kundo Mathew ameyaeleza hayo Bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akijibu swali la mbunge wa jimbo la Bunda, Mh. Boniphace Mwita Getere, aliyeuliza ni lini mradi wa maji wa Ziwa Victoria kutoka Butiama kwenda Nyamuswa – Bunda utakamilika.
Kuhusu hatua za mradi huo zilizokamilika mpaka sasa, Naibu Waziri, Mhandisi Mathew amelieleza Bunge kuwa, Serikali imekamilisha usanifu wa mradi wa maji wa Ziwa Victoria ambao utatoa maji kwenye tanki la lita 2,000,000 la mradi wa Mugango-Kiabakari lililoko Wilaya ya Butiama kwenda Bisarye mpaka Nyamuswa wilayani Bunda mkoani Mara.
Mhandisi Kundo Mathew, aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo unatarajiwa kuanza mwaka wa fedha 2024/25 ambapo kazi zinazotarajiwa kutekelezwa ni pamoja na ujenzi wa matanki mawili (2) yenye jumla ya ujazo wa lita 500,000, ulazaji wa bomba umbali wa kilomita 23.1, ukarabati wa vituo 18 vya kuchotea maji pamoja na kuunganisha zaidi ya wateja 2,000 wa majumbani.