Naibu Waziri wa Maji, Mh. Mhandisi Kundo Mathew ameliambia Bunge jijini Dodoma kuwa, Serikali kupitia Mamlaka ya Maji na Usafi wa mazingira Arusha (AUWSA) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa miundombinu ya uondoshaji majitaka wa Olmoti utakaonufaisha Kiwanda cha A to Z pamoja na wakazi 1,200 wa maeneo hayo.
Naibu Waziri, Mhandisi Mathew, amebainisha hayo Bungeni, jijini Dodoma wakati akitolea majibu swali lililoulizwa na mbunge wa jimbo la Arusha Mjini, Mh. Mrisho Gambo aliyetaka kufahamu ni lini mradi wa majitaka uliopo kata ya Olmot ambao utaunganishwa na kiwanda cha A to Z utakamilika.
Akitolea ufafanuzi zaidi juu ya kazi mbalimbali zinazotekelezwa na mradi huo, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Mathew amesema ni pamoja na ulazaji wa mabomba umbali wa kilomita 11.8, ujenzi wa nguzo 30 za kushikilia bomba kwenye vivuko na ujenzi wa chemba 125 za ukaguzi wa mfumo wa majitaka.
Akilezea makadiro na matarajio ya kukamilika kwa mradi huo mkubwa, unaotekelezwa na Serikali ya awamu ya Sita, kwa maelezo mahsusi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Mhandisi Mathew, ameliarifu Bunge kuwa hadi sasa utekelezaji wa mradi huo umefikia wastani wa asilimia 40 na unatarajiwa kukamilika mwezi Desemba, 2024.