Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuimarisha miundombinu ya Chuo cha VETA Kitangali mwaka hadi mwaka ambapo jengo jipya la utawala lilijengwa na kukarabati baadhi ya majengo ili kupata karakana mbili za ushonaji na umeme, darasa pamoja na bweni.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Mh. Omar Kipanga amelieleza Bunge kuwa katika mwaka wa fedha 2023/24, Serikali imeendelea kuboresha miundombinu ya chuo kwa kujenga bweni la wasichana pamoja na nyumba ya Mkuu wa Chuo.
Akiongeza maelezo zaidi ya uwekezaji uliofanywa na Serikali katika chuo hiko, Naibu Waziri Mh. Kapinga amelitaarifu Bunge kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25, kiasi cha shilingi milioni mia moja (100,000,000) kimetengwa kwa ajili ya umaliziaji wa miundombinu hiyo.
Mh. Kipanga alilihakikishia bunge kuwa kwa kuzingatia upatikanaji wa fedha, Serikali itaendelea kutenga bajeti kwa ajili ya kuongeza miundombinu mingine ya majengo ikiwemo mabweni na karakana katika chuo hicho.