728 x 90

Serikali Kuendelea Kutoa Ruzuku Ya Mbolea Kwa Wakulima Nchi Nzima.

  • June 21, 2024
Serikali Kuendelea Kutoa Ruzuku Ya Mbolea Kwa Wakulima Nchi Nzima.

Naibu Waziri wa kilimo Mh. David Silinde ametoa msimamo wa Serikali kuhusiana na mikakati ya Serikali kukabiliana na ongezeko la bei ya pembejeo nchini.

Mh. Silinde amesema azma ya Serikali ni kuendelea kufanya jitihada za makusudi kuhamasisha kilimo chenye tija nchini kwa madhumuni ya kukuza uchumi wa nchi na kuboresha vipato vya wananchi.

Akijibu swali bungeni la Mh. Stella Simon Fiyao (Viti Maalum) aliyetaka kujua Serikali imejipanga vipi kukabiliana na ongezeko la bei ya pembejeo za kilimo, Mh. David Silinde alizitaja hatua mbalimbali ambazo zimeanza kuchukuliwa na Serikali.

Mosi, Mh. Silinde amesema kuwa Serikali imeanza kutoa ruzuku ya mbolea kwa wakulima wa mazao yote hapa nchini ili kuwapa unafuu wa bei ya mbolea, kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza upatikanaji wa malighafi za viwanda vya ndani.

Mbali na hapo, Mh. Naibu Waziri wa Kilimo, aliongeza kuwa, Serikali imeendelea kuratibu ununuzi wa pamoja wa pembejeo za mazao ya korosho pamba na tumbaku kwa kuagiza moja kwa moja kutoka kwenye chanzo cha uzalishaji.

Mh. David Silinde ameongeza kuwa Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuhamasisha kampuni za pembejeo kutumia reli kusafirisha pembejeo kwenda mikoani ili kupunguza gharama za usafirishaji.

Naibu Waziri Silinde ameitaja hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali katika jitihada za kukabiliana na ongezeko la bei za pembejeo za kilimo kuwa ni kuhamasisha sekta binafsi kuwekeza katika uzakishaji wa pembejeo za kilimo nchini ili kupunguza utegemezi wa kuagiza kutoka nje ya nchi.

Hatua nyingine iliyotajwa kupitia majibu ya Serikali juu ya hatua inazozichukua kukabiliana na ongezeko la bei za pembejeo za kilimo ni kuanisha na kutangaza bei elekezi za mbegu bora kila mwaka ili kudhibiti upandaji holela wa bei za mbegu.

Naibu Waziri wa Kilimo Mh. David Silinde, ametamka kuwa Serikali itaendelea kushirikisha sekta binafsi kuwekeza katika uzalishaji wa mbegu ndani ya nchi kwa kuingia mikataba ya muda mrefu na wakala wa mbegu za kilimo (ASA) na TARI ili kuzalisha mbegu bora kwa kutumia mashamba ya Serikali.