Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekusudia kuongeza idadi ya walimu nchini kwa mwaka huu wa fedha wa 2023/2024. Lengo la Serikali mbali na kupandisha ubora wa elimu, ni kuhakikisha kunakuwa na uwiano mzuri wa mgawanyo wa walimu kwa mikoa yote, kwa kuzingatia mahitaji mahsusi ya kila mkoa.
Akitolea ufafanuzi swali la Mh. Juliana Shonza Mbunge wa viti maalum mkoa wa Songwe, Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais, TAMISEMI Mh. Zainab Katimba amesema serikali inatambua umuhimu wa walimu wa kike katika malezi ya wanafunzi pamoja na uhitaji wa walimu wa masomo ya sayansi.
Katika kutatua changamoto hizo, katika mwaka 2023/24 serikali inatarajia kuajiri walimu 12,000 wa kike na wa kiume wa masomo yote yakiwemo ya sayansi ambao watapangiwa vituo mbalimbali ikiwemo na Mkoa wa Songwe.