728 x 90

Rais Samia Suluhu Hassan aagiza huduma za kijamii ziboreshwe Ngorongoro.

  • August 23, 2024
Rais Samia Suluhu Hassan aagiza huduma za kijamii ziboreshwe Ngorongoro.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa maagizo kwa watendaji wa Serikali yake kuhakikisha huduma zote za kijamii zilizositishwa zikiwemo za afya na shule katika Tarafa ya Ngorongoro Mkoani Arusha zinarudishwa na kuboreshwa haraka iwezekanvyo.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda ameagizwa kusimamia zoezi hilo la kuhakikisha wananchi wa Kata hiyo ya Ngorongoro wanafikiwa na huduma hizo ili kutunza utu wao kupitia huduma hizo za msingi.

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amewatoa hofu wananchi wa Ngorongoro juu ya mashaka waliyokuwa nayo ya uwezekano wa kutokufanyika kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa kama ulivyotangazwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI Mhe. Mohamed Mchengerwa. Mhe. Dkt. Samia amewahakikishia wananchi hao kuwa Uchaguzi huo uliopangwa kufanyika tarehe 27 November mwaka huu utafanyika kama ulivyopangwa awali.

Wananchi hao wa Ngorongoro ambao shauku yao kubwa ilikuwa ni kukutana na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan wamepokea kwa nderemo na vifijo ahadi ya Mhe. Rais Dkt. Samia kuwa atapanga ziara ya kufika Ngorongoro na kuzungumza nao.

Katika kuhakikisha maagizo ya Mhe. Rais yanafanyiwa kazi mara moja, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda amemuahidi Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) kusimamia utekelezaji wa maagizo hayo upesi.

Mhe. Makonda ametumia Mkutano huo kuwashukuru wananchi hao waliojitokeza kueleza kero zao huku akiwapongeza kwa ukomavu waliouonyesha wa kujieleza kistaarabu. Makonda amewatoa hofu wananchi hao kuwa hakuna hata mmoja atakaekosa huduma ya msingi.