Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametoa msisitizo kwa viongozi wa umma, kuwathamini na kuwaheshimu wananchi. Rais Dkt. Samia ameyasema hayo leo tarehe 26 Julai 2024 Ikulu jijini Dar es salaam alipokuwa akiwaapisha wateule wake wa nafasi mbalimbali kwenye Serikali yake.
Rais Dkt. Samia amewataka viongozi wote wa umma kusimamia viapo walivyoapa mbele ya Mamlaka iliyowateua na mbele ya wananchi wanaokwenda kuwatumikia kwa kuhakikisha maslahi ya wananchi yanapewa kipaumbele.
Rais Samia Suluhu Hassan amewakumbusha viongozi hao aliowaapisha ambao ni pamoja na Mawaziri, Naibu Mawaziri, Katibu Mkuu, Makatibu Tawala wa Mikoa pamoja na Balozi, kuwa madaraka waliyonayo ni dhamana inayotakiwa kufanyiwa kazi na uwajibikaji inaoendana na mwenendo, matendo na kauli njema.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliitumia hafla hiyo ya uapisho ambayo pia ilihudhuriwa na Makamu wa Rais, Dkt. Phillip Mpango, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Naibu Spika, Musa Zungu, kuwaonya watumishi wa umma kuepukana na utovu wa nidhamu usioakisi hulka ya utanzania na heshima inayoendana na nafasi wanazoaminiwa kuzitumikia.
Rais Samia aliitumia fursa hiyo kutoa maagizo ya kisekta kwa Mawaziri aliowaapisha, yanayolenga kuimarisha na kuboresha ufanisi wa huduma za msingi zinazokusudia kugusa maisha ya watanzania, kama uratibu mzuri wa ajira kwa vijana nchini, kasi ya uimarishwaji wa mawasiliano nchini na muendelezo wa utatuzi wa kero za ardhi.
Rais Samia aliendelea kuwakumbusha viongozi hao kwamba madaraka ni sawa na nguo ya kuazima ambayo wakati wowote Mmiliki wa nguo anaweza kuichukua.