Rais wa Jamhuri ya Muungano ya Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kuweka historia ya kuwa Rais mwenye mafanikio zaidi katika soka la Tanzania. Kuelekea mchezo wa kuwania tiketi ya kufuzu kucheza kombe la dunia, Rais Dkt. Samia Suluhu alitoa ahadi nono ya milioni 100 kwa wachezaji wa Taifa Stars, kama wangeshinda mchezo huo.
Ahadi hiyo iliyotangazwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro kwa niaba ya Rais Dkt. Samia, imekua chachu kubwa kwa Taifa Stars ya kuvuna pointi zote tatu ikiwa ugenini. Rais Dkt. Samia amekuwa na muendelezo mzuri wa kutoa hamasa kwa timu za michezo nchini, hali inayopelekea kuongezeka kwa ari na shauku ya mafanikio kwa timu za Tanzania.
Ahadi hiyo imekuja baada Rais Dkt. Samia kujizolea umaarufu mkubwa kupitia “Goli la Mama” ambalo amekuwa akiahidi kwa vilabu vya Tanzania vinavyoshiriki mashindano ya kimataifa.
Ushindi huo mkubwa katika historia ya Tanzania ni kielelezo cha uwekezaji mkubwa uliofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sekta ya michezo. Chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia, Tanzania iliingiza kwa mara ya kwanza timu mbili katika hatua ya robo fainali ya Klabu Bingwa barani Afrika. Mbali na hapo timu za taifa za wanawake na za vijana zimefanya vizuri katika awamu hii ya sita kuliko nyingine zote zilizopita.
Katika harakati za kuinua Utamaduni, Sanaa na Michezo nchini, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameahidi kuendelea kujitoa ili kuharakisha mafanikio zaidi kwenye sekta ya michezo nchini. Rai kubwa ya Mh. Dkt. Samia Suluhu ni wadau wa michezo kuendelea kushikamana ili kuchochea mafanikio zaidi nje ya mipaka ya Tanzania.
Mh. Dkt. Samia Suluhu ameendelea kuonyesha kwa vitendo, upendo wake kwa sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo baada ya hivi karibuni kusafiri na baadhi ya wasanii na watayarishaji wa filamu kwenye ziara yake ya kikazi nchini Korea iliyokuwa na tija kubwa ya kuhamasisha ushirikiano wa kimkakati baina ya watu tasnia hiyo wa Tanzania na Korea.
Ushindi wa Taifa Stars ilioupata nchini Zambia ni zawadi kwa Rais Dkt. Samia kwa mchango wake kaitika safari ya kutafuta tiketi ya kufuzu kombe la dunia. Kwa kasi hii ya muendelezo wa matokeo mazuri, ni wazi taifa la Tanzania litaendelea kunufaika zaidi kwa Rais Dkt. Samia kuendelea kuaminiwa na kuungwa mkono na wadau wa sekta mbalimbali nchini.