728 x 90

Rais Samia aweka rekodi kubwa kwenye sekta ya utalii nchini.

  • June 4, 2024
Rais Samia aweka rekodi kubwa kwenye sekta ya utalii nchini.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameingia katika vitabu vya kumbukumbu za historia kwa mchango wake kwenye sekta ya utalii nchini.

Ikumbukwe kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliingia madarakani kwenye kipindi ambacho dunia nzima ilikua inapitia katika hali ngumu ya mdororo wa kiuchumi uliochagizwa na janga la uviko 19.

Wakati Dkt. Samia anachukua uongozi wa nchi, sekta ya utalii ilikuwa miongoni mwa sekta zilizokuwa katika hali mbaya zaidi nchini kutokana na ufinyu wa wageni waliokuwa wakiingia nchini, hali iliyopelekea upotevu mkubwa wa ajira kwa vijana wa kitanzania na kushuka kwa mchango wa sekta ya utalii katika pato la taifa.

Kazi kubwa ya Dkt. Samia ilikua kusuka mpango madhubuti na mkakati wa kisayansi ulioshirikisha wabobevu wa sekta ya utilii nchini na ulimwenguni, kama msingi wa kuja suluhisho la kuiponya sekta ya utalii.

Shauku kubwa ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ilikua kurudisha ajira za vijana wa kitanzania zilizopotea kwa kurudisha imani kwa watalii kutoka nje ya nchi lakini pia kuhamasisha utalii wa ndani.

Takwimu zinaonyesha uwepo wa ongezeko kubwa la watalii kutoka nje ya Tanzania, ambapo mwaka 2021 takribani watalii 922,692 walikadiriwa kuja kutalii nchini. Mwaka 2023 kulikuwa na ongezeko maradufu la watalii ukilinganisha wale wa 2021 ambapo takriban watalii milioni mbili waliingia Tanzania.Hilo ongezeko ni sawa na asilimia 96%.
Watalii wengi kati ya hao ilikuwa ni mara yao ya kwanza kuja Tanzania huku wakielezea kuvutiwa na filamu ya Royal tour iliyomhusisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikiwa kuchochea ukuaji wa utalii wa ndani tofauti na ilivyokuwa kabla. Takwimu za mwaka 2021 zionyesha takriban watalii 788,933 wa ndani walitembelea vivutio mbalimbali hapa nchini. Baada ya Dkt. Samia Suluhu kuasisi filamu ya Royal tour, iliyokuwa na maudhui ya kutangaza vivutio mbalimbali vinavyipatikana nchini, kulikuwa na ongezeko kubwa la watalii wa ndani mwaka 2023 waliokadiriwa kufika 1,985,707 sawa na ongezeko la asilimia 152%.

Kiu kubwa ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwekeza kwenye utalii ilikuwa kuongeza mchango wa sekta hiyo kwenye pato la taifa. Mwaka 2021 mchango wa sekta ya utalii kwa pato la taifa ulikuwa bilioni 46.3 za kitanzania. Jitihada za Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan zilifanikisha ongezeko la bilioni 175.3 ilipofika mwaka 2023, ambayo ni ongezeko la asilimia 279% kulinganisha na mwaka 2021.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amehakikisha wananchi wake waliopata madhara kutoka kwa wanyama pori wakali na waharibifu wa mali na mazao wanafidiwa ipasvyo. Kufikia mwezi Julai 2023, jumla ya Shilingi bilioni 2.4 zililipwa kwa wananchi 10,552 wa halmshauri za wilaya 48 nchini.

Chini ya usimamizi yakinifu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, taswira ya ukuaji wa utalii nchini imebebwa na uwepo wa ongezeko wa mapato yatokanayo na utalii kimataifa. Pato hilo limeongezeka kutoka USD bilioni 1.3 mwaka 2021 mpaka kufikia USD bilioni 3.4 mwaka 2023. Hilo ni ongezeko la asilimia 161.

Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiwezesha sekta ya utalii nchini kushinda tuzo nyingi za kimataifa kwa kuhamasisha ongezeko la ubora kwa watoa huduma za utalii na uwekaji wa mazingira rafiki ya kuvutia watilii kama ununuzi wa ndege za kisasa za abiria unaowarahisishia watalii kufika Tanzania kwa wepesi. Kwenye awamu hii ya sita inayoongozwa na Mh. Dkt. Samia, Tanzania imeshika nafasi ya 12 duniani kote na ya pili Barani Afrika kwa ongezeko la watalii ikilinganishwa na vipindi kama hivyo kuanzia mwaka 2019 mpaka 2023.

Mafanikio haya makubwa ni matokeo ya imani kubwa watanzania waliyonayo kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan. Uzalendo wake unadhihirisha dhamira yake ya uwazi ya kuboresha maisha ya watanzania wote.