Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan, ameonyesha hali ya kufurahishwa na ukuaji wa michango ya Mashirika na Taasisi za Umma kupitia magawio waliyotoa kwa Serikali leo jijini Dar es Salaam.
Mashirika na Taasisi za Umma Kutoa Gawio
Akihutubia umma wa Watanzania kupitia viongozi mbalimbali wa Serikali, Rais Samia ameridhia ombi la Msajili wa Hazina, Ndg. Nehemia Mchechu, la kutenga siku maalum kila mwaka kwa Mashirika na Taasisi za Umma kutoa gawio kwa Serikali.
Rais Samia alifafanua kuwa lengo la hatua hii ni kuzifanya Taasisi na Mashirika ya Umma kukumbuka wajibu wao kwa jamii ya Watanzania ambao wanawekeza kupitia kodi.
Jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita
Rais Samia alisisitiza kuwa Uongozi wa Awamu ya Sita umejikita katika kutengeneza sera zinazowezesha mazingira rafiki kwa ukuaji na ustawi wa uwekezaji, pamoja na uboreshaji wa huduma za jamii.
Aliwahimiza wenyeviti wa bodi za Mashirika na Taasisi ambazo hazikutoa gawio au zilitoa gawio chini ya kiwango kilichowekwa kisheria kuhakikisha wanawasilisha gawio kwa Serikali kabla ya mwaka wa fedha wa 2024 kumalizika.
Maagizo kwa Wakuu wa Mashirika na Taasisi
Rais Samia aliagiza wakuu wa Mashirika na Taasisi zote zenye hisa za Serikali kuhakikisha wanajifungamanisha na mifumo ya Serikali ili isomane kama ilivyofanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Bandari (TPA).
Michango ya Mashirika na Taasisi kwa Serikali
Katika hafla hiyo, Rais Samia alipokea kwa niaba ya Serikali, jumla ya shilingi 637,122,914,887.59 kutoka kwa Mashirika na Taasisi 145 kama michango na gawio. Kati ya hizo, gawio lilikuwa shilingi 278,868,961,122.85 kutoka Mashirika ya Biashara huku shilingi 358,253,953,764.74 zikitoka kwenye Taasisi nyingine.