Msimu wa Ligi Kuu ya soka Tanzania bara 2023/2024 umetamatika rasmi kwa Klabu ya Yanga ya Dar es salaam kutwaa ubingwa wa ligi hiyo. Katika hali nyingine isiyozoeleka, Klabu ya Azam ya jijini Dar es salaam imekamata nafasi ya pili mbele ya klabu kongwe nchini Simba S.C.
Kivutio kingine msimu wa 2023/2024 kilikuwa ni Klabu ya Costal Union ya jijini Tanga iliyofuzu kushiriki michuano ya kimataifa kwa kushika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi kuu.
Kwa mara ya kwanza kwa miaka mingi msimu huu umeshuhudia anguko la moja ya timu kongwe Mtibwa Sugar iliyoshuka daraja kutokana na muendelezo mbovu wa kimatokeo. Mabingwa hawa wa zamani wa Tanzania bara watashiriki championship msimu ujao kataika harakati za kuirudisha heshima yao iliyopotea msimu huu.
Msimu huu wa 2023/2024 ulitoa burudani kubwa pia katika mbio za ufungaji bora kwa wachezaji Waziri Junior wa Kmc, Feisal Salum wa Azam na Aziz Ki wa Yanga kuchuana vikali. Mpaka kuelekea michezo ya mwisho wa ligi Aziz ki na Feisal walikuwa wamelingana idadi ya magoli waliyofunga, 18. Ni katika mchezo wa mwisho ndio mbabe kati yao alipofahamika kwa Aziz ki kufunga magoli matatu na kufikisha magoli 21, huku Feisal akiongeza moja na kufikia magoli 19.
Kibarua kingine katika msimu wa soka wa 2023/2024 kilikuwa kwa wakufunzi wazawa dhidi ya wageni. makocha wa kigeni wameendelea kuitawala ligi kuu ya Tanzania kwa idadi ya dhidi ya wazawa, huku kukiwa na kocha mmoja tu mzawa aliyeiwezesha timu yake kushika moja kati ya nafasi nne za juu katika msimamo.
Changamoto za uamuzi wa michezo zimeendelea kukithiri kwa waamuzi wa Ligi Kuu ya nbc huku kukiwa na wasiwasi kwa wadau wengi kuwa huenda tiba isipatikane karibuni. Matukio tata yameendelea kushamiri. Kitendo kinachotafsiriwa na wengi kama udhaifu mkubwa wa ligi hii ya nbc.
Moja kati ya mambo ya kusifiwa kwa msimu huu wa 2023/2024 ni utulivu wa ratiba ambayo tofauti na miaka mingine, haikuwa na viporo. Kwa kiasi kikubwa bodi ya ligi walijitahidi kuendana na kalenda za FIFA na zile za CAF, japo TFF walishawishika kuishirikisha timu ya taifa katika mashindano yasiyo rasmi kule Mongolia, hali iliyopelekea baadhi ya vilabu kugomea kutoa wachezaji wao.
Ubora wa wachezaji wa kigeni ni kitu kingine ambacho kimekuwa na mvuto wa kipekee msimu huu. Ni wazi kuwa ligi yetu sasa imeanza kuwa na mvuto wa aina yake kwa wachezaji wengi wa daraja la kati kutoka mataifa mengi ya Afrika n ahata nje ya Afrika. Ligi yetu kuwa na mchezaji kutoka Colombia ni upekee ambao haupatikani kwingineko Afrika Mashariki na Kati.
TFF kwa kushirikiana na serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuboresha miundombinu na kuvutia wawekezaji mbalimbali kama Azam Media, Nbc na wengineo kwa nia ya kuikuza ligi kupitia uwekezaji wa nyenzo za kisasa na maboresho ya sera na miundombinu.
Ukuaji wa kiwango cha ligi yetu unapimika pia kwa ushiriki madhubuti wa timu za simba na yanga katika mashindano ya kimataifa, ambapo timu zote mbili zilifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali kwenye michuano ya klabu bingwa barani Afrka.
Kwa namna ya kipekee kabisa, ubora wa msimu huu umechagizwa na ushiriki wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyechagiza ushindani kupitia hamasa zake za goli la mama.