Kasi ya upatikanaji wa vitambulisho vya nida imezidi kuongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na msukumo wa Serikali ya awamu ya Sita.
Akijibu swali la mbunge wa Moshi Mjini, Mh. Priscus Tarimo, aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani wa kuharakisha mchakato wa upatikanaji wa vitambulisho vya Taifa unaokwenda taratibu sana, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Daniel Barran Sillo amesema kwa mwaka huu uzalishaji wa vitambulisho umeongezeka kutokana na uimarishwaji wa NIDA ulifanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kununua vifaa vya kisasa zaid kwa ajili ya kuongeza ufanisi.
Akitoa maelezo zaidi, Naibu Waziri Sillo amefafanua kuwa tayari mpaka sasa nida imezalisha jumla ya vitambulisho 21,322,098 ambayo ni sawa na asilimia 86 ya wananchi 24,818,138 waliosajiliwa.
Naibu Waziri Sillo ameongeza kuwa vitambulisho 20,340,713 vimekwisha sambazwa kwenye ofisi za usajili za wilaya, Serikali za Mitaa, Vijiji na Shehia kote nchini.
Akitoa takwimu za Serikali, Mh. Sillo ameliambia bunge kuwa kati ya vitambulisho hivyo, vitambulisho 19,139,601 sawa na asilimia 94 vimeshachukuliwa na wananchi.
Naibu Waziri Sillo alitumia sehemu ya majibu ya swali hilo kutoa rai kwa wananchi wote ambao bado hawajachukua vitambulisho vyao vya Taifa kufika katika ofisi za Serikali za Mitaa na Vijiji walipojiandikisha kwa ajili ya kuchukua vitambulisho vyao.