728 x 90

Je, Serikali inafanya nini kuilinda jamii dhidi ya athari hasi za michezo ya kubahatisha (Kamari)?

  • June 24, 2024
Je, Serikali inafanya nini kuilinda jamii dhidi ya athari hasi za michezo ya kubahatisha (Kamari)?

Naibu Waziri wa Fedha Mh. Hamad Chande ameliambia Bunge kuwa, pamoja na faida za kiuchumi zinazotokana na michezo ya kubahatisha, Serikali inatambua athari hasi katika jamii endapo michezo hiyo haitaendeshwa kwa weledi.

Mh. Chande ameyasema hayo alipokuwa akilitolea maelezo swali la Mh. Ng’wasi Damas Kamani aliyetaka kujua, Serikali ina mkakati gani wa kupambana na uraibu wa mchezo wa kamari unaoongezeka kwa kasi kwa vijana.

Naibu Waziri wa fedha, Mh. Chande amelieleza bunge jijini Dodoma kuwa, bodi ya michezo ya kubahatisha ina jukumu la kuhakikisha kuwa jamii inalindwa ipasavyo dhidi ya athari hasi za michezo ya kubahatisha. Naibu Waziri huyo aliongezea kuwa bidi hiyo imepewa mamlaka hayo kwa mujibu wa kifungu cha 7(2)(i) cha sheria ya michezo ya kubahatisha SURA 41.

Naibu Waziri wa fedha alitaja mikakati hiyo inayochukuliwa na bodi hiyo kuwa ni pamoja na kuimarisha udhibiti na uratibu wa sekta hiyo kwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwa waendeshaji.

Mbali na hapo, Naibu Waziri wa Wizara ya Fedha, Mh. Hamad Chande aliliambia bunge kuwa, Serikali inaendelea na zoezi la kutoa elimu kwa jamii na wadau mbalimbali kuhusu athari hasi za michezo ya kubahatisha.

Ili kuondoa na kudhibiti tatizo hilo la uraibu wa michezo ya kubahatisha, Mh. Hamad Chande amelitaarifu bunge kuwa Serikali imeendelea kutoa maelekezo na kusimamia utekelezaji wake kwa waendeshaji wa michezo ya kubahatisha kuhusu kuchukua hatua mbalimbali za kuilinda jamii ikiwemo kuwazuia wachezaji wanaobainika kuelekea katika uraibu.

Mkakati mwingine ambao Serikali ya awamu ya Sita imeendelea kuuwekea mkazo ili kudhibiti na kuzuia mfumuko wa uraibu kwa mujibu wa Naibu Waziri Chande ni kuzuia na kudhibiti michezo ya kubahatisha isiyo na usajili ambayo ni chanzo kikubwa cha athari mbaya kwa jamii.

Hatua nyingine ambayo imetajwa na Naibu Waziri Chande ni Serikali kuendelea kusimamia utekelezaji wa sera ya watoa habari yenye lengo la kuishirikisha jamii kutoa taarifa kuhusiana na michezo ya kubahatisha ikiwemo waendeshaji haramu, ushiriki wa watoto chini ya umri wa miaka 18, na ushiriki uliopitiliza.