728 x 90

Bilioni 1.2 Kujenga Stendi Liwale.

  • June 21, 2024
Bilioni 1.2 Kujenga Stendi Liwale.

Swrikali ya awamu ya Sita, imetenga kiasi cha shilingi bilioni 1.2 kwa ajili ya kujenga mradi wa kimkakati wilayani Liwale, kama sehemu ya kitega uchumi cha kukuza mapato ya halmashauri hiyo.

Hatua hiyo imetajwa kama jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuziongezea halmashauri uwezo wa kuvutia uwekezaji na kutanua wigo wa ukusanyaji wa mapato.

Hadi kufikia mwezi February 2024, tayari Serikali ilishawasilisha kiasi cha shilingi milioni 452.8 kwa ajili ya ujenzi wa stendi hiyo ya kisasa. Fedha hizo, kulingana na maelezo ya Naibu Waziri wa fedha Mh. Hamad Chande, zimetolewa kulingana na madai yaliyowasilishwa kulingana na mpango kazi.

Kupitia majibu yake Bungeni jijini Dodoma, alipokuwa akijibu swali la mbunge wa Liwale Mh. Zuberi Mohamedi Kachauka, aliyetaka kufahamu Serikali ina mpango gani kuirejeshea halmashauri ya Liwale fedha za kutekeleza miradi ya kimkakati iliyorudishwa hazina ili iweze kujenga stendi ya kisasa, Naibu Waziri Chande aliongeza kuwa, katika mwaka ujao wa fedha 2024/25 kiasi cha shilingi milioni 412.8 kimetengwa kwa ajili ya mradi huu. Mh. Chande aliendelea kusisitiza kuwa kwa shughuli ambazo hazikutekelezwa kulingana na mkataba kutokana na sababu mbalimbali, halmashauri ya wilaya ya Liwale inaelekezwa kutenga bajeti ya kugharamia shughuli hizo.

Akimalizia kulitolea ufafanuzi swali hilo, Naibu Waziri Chande amesema kuwa azma ya Serikali ni kuhakikisha kuwa mradi wa stendi ya kisasa ya Liwale unatekelezwa kulingana na mkataba ulivyopangwa.