Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, ni miongoni mwa viongozi wakuu waliohudhuria tukio muhimu katika Ikulu ya Nairobi, ambapo Rais wa Kenya, William Ruto, alimuidhinisha rasmi Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kwa nafasi ya Uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Kenya imeweka nafasi ya Bw. Odinga kama mwakilishi wa maslahi ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), badala ya Kenya pekee. Hatua hii iliimarishwa zaidi na kujiondoa kwa aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Somalia, Fawzia Yusuf, kwenye kinyang’anyiro hicho na kisha kumuunga mkono Bw. Odinga.
Tukio hilo la hadhi ya juu liliwaleta pamoja viongozi kadhaa wa kanda, wakiwemo Rais wa Uganda Yoweri Museveni, Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir, na Rais wa zamani wa Tanzania Jakaya Kikwete. Waziri Mkuu wa Burundi, Gervais Ndirakobuca, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda, James Kabarebe, pia walihudhuria.
Kwa kuonyesha mshikamano wa bara, Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, ambaye hivi karibuni alikuwa na Bw. Odinga katika ufunguzi wa Tamasha la Tano la Dunia la Sanaa na Utamaduni wa Watu Weusi na Waafrika (Festac) huko Kisumu, alikuwepo kutoa sapoti yake.
Mkutano huu unaonyesha uungwaji mkono mkubwa wa kanda kwa nafasi ya Bw. Odinga, na kusisitiza kujitolea kwa viongozi wa Afrika Mashariki katika uwakilishi wa pamoja kwenye Umoja wa Afrika.