Wanaharakati na asasi za kuwatetea watu walioathirika kwa kupigwa kutokana na kuvamia mgodi wa Nyamongo wametupiwa lawama na waathirika hao kwa kujinufaisha wenyewe kupitia maswaibu ya waathirika kwa kujipatia kiasi kikubwa cha fidia inayotolewa na mgodi ikilinganishwa na kiasi wanachopata waathirika.
Mgodi wa dhahabu wa North Mara unaomilikiwa kwa ubia kati ya kampuni ya Barrick Gold na Serikali ya Tanzania kupitia kampuni ya Twiga Minerals Corp umekuwa ukikabiliwa na wimbi la uvamizi kutoka kwa watu wanaolenga kuiba mchanga wenye dhahabu. Wavamizi hawa huiba mchanga mchana kweupe wakitumia silaha za jadi kama mapanga, sime, upinde, mikuki na nyinginezo.
Katika uvamizi huo, baadhi ya wavamizi ama askari huumizwa vibaya na wengine kupoteza maisha. Hali hii inapojitokeza, wanaharakati wa haki za binadamu huingilia kati kuwatetea waathirika hao ili walipwe fidia.
Moja ya kesi maarufu ya aina hiyo ni ile inayomhusu Bwana Samwel Mwita Nyangore, mkazi wa Kijiji cha Siriba, kata ya Sirari, Wilaya ya Tarime, Mkoa wa Mara. Yeye na wenzake walipatwa na mkasa huo baada ya kuvamia mgodi mnamo mwaka 2011, ambapo katika mapambano na askari polisi waliokuwa wanawazuia kufanya uhalifu, Samwel alipigwa risasi na kujeruhiwa vibaya.
Bwana Samwel akiwa hospitalini kwa matibabu, alitembelewa na wanasheria wa Kampuni ya Leigh Day kutoka Uingereza, wakiwa na lengo la kuwasaidia waathirika wapate haki zao. Wanasheria hao walifungua kesi dhidi ya Kampuni ya Acacia Mining, iliyokuwa ikiendesha mgodi wa North Mara wakati huo.
Hata hivyo, kabla ya kesi kumalizika, pande zote mbili zilikubaliana kumaliza kesi nje ya mahakama, na Kampuni ya Acacia Mining ilikubali kuwalipa fidia waathirika hao mnamo mwaka 2015.
Bwana Nyangore, akiwa bado hospitalini akiendelea na matibabu, alieleza kuwa alitembelewa na wanasheria wawili, mmoja mzungu na mwingine Mtanzania, ambao walimpatia hundi ya Tsh milioni 150. Baadaye, alipotoka hospitalini, alibaini kuwa kiasi alichopewa na wanasheria wa Leigh Day kilikuwa kidogo sana ikilinganishwa na kiasi kilicholipwa na Kampuni ya Acacia Mining.
Utafiti uliofanywa na chombo cha habari cha Ujerumani, DW, ulibaini kuwa kiwango kilicholipwa na Acacia Mining kama fidia kwa Bwana Nyangore ni Tsh milioni 387.54, ambapo yeye alilipwa Tsh milioni 150, sawa na asilimia 38.6 ya fidia hiyo.
Samuel Peter Timasi, Mwenyekiti wa asasi ya kijamii (MUCHATA), yenye lengo la kupinga maovu nchini Tanzania, alisema, “Wapigania haki za binadamu kutoka Uingereza na Canada, wanapoendesha hizi kesi za watu wa Nyamongo, hulipwa fedha nyingi sana kama fidia, lakini matokeo yake waathirika wenyewe hupewa fedha kidogo sana ambazo haziendani na madhara wala maumivu waliyoyapata.”
Bwana Timasi alisema kuwa wanaharakati hao, kwa kushirikiana na wanaharakati wa Tanzania, wanatumia udhaifu wa elimu na uelewa mdogo wa waathirika kuwadhulumu haki zao.
Kwa miaka mingi, Kampuni ya Sheria ya Leigh Day imekuwa ikisimamia kesi za watu wanaovamia mgodi kwa nia ya kuiba mchanga wa dhahabu. Hata hivyo, kampuni hiyo imekuwa ikitupiwa lawama kwa kiasi kikubwa kwa kujinufaisha zaidi kupitia kesi hizo kwa kuchukua sehemu kubwa ya fidia inayolipwa kuliko waathirika wenyewe.
Kampuni ya Leigh Day, baada ya kuulizwa, ilikanusha tuhuma hizo na kukataa kutaja viwango wanavyowalipa wateja wao, huku wakisisitiza kwamba ni siri ya kisheria. Kulingana na utafiti uliofanywa kwa waathirika na nyaraka za mahakama zilizopatikana na duru za habari, inaonekana kuwa Leigh Day huchukua kati ya asilimia 60 hadi 70 ya fidia inayolipwa na mgodi.
Kesi hizo mara nyingi huendeshwa nje ya Tanzania, hivyo kutoa urahisi zaidi kwa kampuni hizo kudhulumu haki za waathirika. Mbunge wa Tarime Vijijini, Mheshimiwa Mwita Waitara, anakiri kuwepo kwa malalamiko kutoka kwa waathirika wa matukio hayo.
“Kampuni ya Leigh Day inadai kwamba inatetea wananchi, lakini ni uwongo, bali wao ndio wanaonufaika zaidi na kesi za waathirika,” alisema Mbunge Mwita Waitara.
Mgogoro unaozunguka fidia kwa waathirika wa mgodi wa North Mara umeibua maswali mengi kuhusu uwazi na haki katika mchakato wa fidia. Ingawa wanaharakati na kampuni za sheria wanajitambulisha kama watetezi wa haki za binadamu, tuhuma zinazowakabili zinaonyesha picha tofauti, huku waathirika wakidai kutotendewa haki na kufidiwa kidogo ikilinganishwa na fidia inayotolewa na mgodi. Juhudi zaidi zinahitajika ili kuhakikisha kuwa waathirika wanapata haki stahiki na kwamba mifumo ya sheria na fidia inazingatia uwazi na usawa.