728 x 90

Vimebaki vijiji 151 tu kupata umeme nchini.

  • July 23, 2024
Vimebaki vijiji 151 tu kupata umeme nchini.

Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ameeleza kuwa kuwa kati ya vijiji 12,000 nchi nzima, ni vijiji 151 tu ambavyo bado havijaunganishwa na huduma ya umeme.

Kupitia ziara yake mkoani Njombe ya kukagua miradi ya nishati pamoja na kasi ya usambazaji wa umeme katika vijiji vya Lubonde na Maweni, Mhe. Kapinga amesema lengo la Serikali ni kuona kila kijiji nchini kinaunganishwa na huduma hiyo muhimu kwa ustawi wa maendeleo ya jamii.

Mhe. Kapinga katika ziara yake hiyo alishuhudia makubaliano ya kimkataba kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Kampuni binafsi ijulikanayo kama Madope ya Mkoani Njombe ya kukabidhi vifaa vya kusambaza umeme kwa shirika hilo.

Mhe. Judith Kapinga, amesema kwenye makubaliano hayo kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ina kiu ya kuona mchango mkubwa zaidi wa sekta binafsi katika maendeleo ya jamii.

Naibu Waziri Kapinga amesema pia mchango wa Kanisa Katoliki katika uwekezaji kwenye sekta mbalimbali nchini una umuhimu mkubwa na ni wa thamani sana hivyo kuwataka waongeze kasi zaidi na ukubwa wa miradi wanayowekeza.

Upande wa Kanisa Katoliki, uliowakilishwa na Askofu wa Jimbo la Njombe Eusebio Kyando, umepongeza juhudi za Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kwa ushirikiano wao pamoja na kutoa fedha zilizowezesha kufanikisha mradi huo kukamilika.

Kampauni ya kuzalisha umeme ya Madope, ni ya kitanzania ambayo inapatikana Wilaya ya Ludewa ambayo asilimia 55 za umiliki wake ni za Kanisa Katoliki Jimbo la Njombe.