Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kutimiza ahadi zilizotolewa kwenye Ilani ya Chama Cha Mapinduzi, ya kutoa kipaumbele kwa sekta ya afya nchini.
Kasi ya ujenzi wa hospitali za rufaa, hospitali za wilaya, zahati na vituo vya afya nchini imeongezeka kwa kasi kubwa ndani ya miaka hii mitatu ambayo Rais Dkt. Samia ameiongoza Tanzania.
Kiini cha Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwekeza fedha nyingi za bajeti kwenye sekta ya afya, ni kuyaenzi kwa kuyaishi maono ya baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere, ya kupambana na maradhi, kwani ni adui wa Taifa.
Kiu ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kusogeza karibu huduma muhimu za afya kwenye maeneo ya karibu na wananchi.
Kutokana na hulka ya Rais. Dkt. Samia kuwajali wananchi wake, ameelekeza nguvu zake katika kuwaondolea wananchi wake kutumia gharama nyingi kufuata huduma za afya umbali mrefu na badala yake, kuwekeza katika kuhakikisha kila wilaya nchini inakua na hospitali yenye hadhi, na uwezo wa kimiundombinu na kiutaalam wa kutoa huduma bora kwa wananchi.
Lengo la Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia ni kutoa fursa kwa kila mtanzania kuweza kutimiza malengo yake kupitia uhakika wa kupata matibabu ya viwango vikubwa popote pale watakapokuwepo.
Mbali na kujenga hospitali za kisasa na kuziwezesha kuwa na vifaa vinavyomudu kutoa huduma za kibingwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameelekeza uhamasishaji mkubwa sana wa kuwahimiza watanzania, hasa wa sekta zisizo rasmi, kukata bima za afya zinazoratibiwa na mpango wa Serikali wa bima za afya kwa wote, ili kuondokana na ukali wa gharama pindi wanapohitaji matibabu.
Akiwa ziarani mkoani Rukwa, ambapo alipokelewa na Mkuu wa Mkoa huo Mh. Makongoro Nyerere alieambatana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mh. Mohamed Mchengerwa (Mb) na Naibu Waziri wa Afya, Mh. Dkt. Gowin Mollel (Mb), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, alizindua Hospitali ya Wilaya ya Nkasi ambayo imegharimu zaidi ya shilingi za kitanzania bilioni 5.4.
Hospitali hiyo ambayo ni ya kipekee, inauwezo wa kuhudumia watu zaidi ya wale waishio Nkasi, kutokana na kusheheni vifaa na mashine za kisasa, pamoja na wabobevu mahiri waliohitimu katika vyuo bora vya mafunzo ya afya, na wenye uzoefu mkubwa.
Ujenzi wa hospitali hiyo umeondoa adha ya muda mrefu iliyokuwa inawalazimu wananchi wa Nkasi kusafiri masafa marefu kutafuta huduma za afya.
Rais Dkt. Samia ambae kwenye ukaguzi huo alionyesha kufurahishwa na kuridhishwa na matumizi ya pesa yaliyoendana na ubora wa hospitali, alitumia pia wasaa huo kuwahimiza wasimamizi wa hospitali hiyo kutanguliza uzalendo na weledi katika kutoa huduma kwa watanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, wakati akiwasalimu maelfu ya wananchi wa mkoa wa Rukwa waliojitokeza kumlaki, aliwahakikishi kuwa, licha ya maendeleo kuwa na kawaida ya kuhitaji muda, uwekezaji wa Serikali anagoingoza kwenye sekta ya afya utandelea kuwa kipaumbele mpaka pale kila mtanzania atakapokuwa na uhakika wa kuhudumiwa kikamilifu bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.
Ni wazi kuwa dhamira ya dhati ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan juu ya mustakabali wa hufuma za afya nchini, imeanza kutoa mwanga wa matumaini na hakika ya makubwa yatarajiwayo.