Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuweka Jiwe la Msingi kwenye Chuo cha Veta Sumbawanga, akiwa katika ziara yake ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Uwekaji wa jiwe la msingi katika chuo hicho ni alama ya ushindi kwa vijana wa Tanzania, unaotoa tumaini jipya la ukombozi wa kifikra na kimaandalio, katika kujibu swali la ajira kwa vijana nchini.
Msingi wa maono ya Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kubadili mtazamo wa elimu ya Tanzania kutokuwa kuwa ya nadharia na kuifanya elimu ujuzi. Lengo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan, ni kuwapa thamani vijana wa kitanzania ya kuwa na ujuzi utakaowawezesha kuwa sehemu ya masuluhisho ya changamoto zinazoikumba jamii, na kupitia njia hiyo kujikwamua kiuchumi.
Chuo hiko ambacho Serikali imegharamia zaidi ya shilingi za kitanzania bilioni 3.1 kitakuwa na uwezo wa kupokea wanafunzi zaidi ya 1,500 kwa wakati mmoja. Wanufaika wa mafunzo ya vitendo kupitia chuo hiko wanatazamiwa kutokea sehemu mbalimbali zaidi ya Sumbawanga kutokana na uwezo utakaokuwa nao chuo hiko wa kupokea idadi kubwa ya wanafunzi kwa mara moja.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuusuka upya mfumo na utaratibu wa elimu nchini Tanzania, lengo likiwa kuzalisha vijana wenye elimu ya nadharia, lakini pia umahiri wa fani za ufundi mbalimbali ili kuongeza uwezo wa kuajirika na kujiajiri.
Kusudi kuu la Serikali ya awamu ya Sita chini ya uongozi wa Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuwezesha upatikanaji wa miundombinu shindani yenye nyenzo za msingi za kuzalisha wabobevu wa fani mbalimbali kama makenika, umeme, ushonaji, usafiri na usafirishaji, usindikaji na nyingine nyingi.
Ili kuongeza hamasa ya vijana kujiunga na mafunzo yanayotolewa kwenye vyuo hivi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Samia Suluhu Hassan, alitoa maelekezo mahsusi kwa Wizara ya Fedha, kuongeza fungu kwenye Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuanza kuangalia namna ya kuwawezesha vijana watakaojiunga na vyuo hivi.
Chuo cha Veta Sumbawanga kitakwenda kujibu moja kwa moja swali la ajira nchini kwa wakazi wa mkoa wa Rukwa kwa kutoa mafunzo ya umahiri kwa vijana wa mkoa wa Rukwa na mikoa ya pembezoni, na kusimamia ubunifu unaolenga kuchangamsha ukuaji wa uchumi nchini. Chuo hicho pia kitajihusisha na uratibu wa mafunzo ya muda mrefu na mfupi ya kukazia maarifa kwa watu wa Rukwa wanaojihusisha na fani mbalimbali ambao hawakupitia mafunzo yeyote kabla.
Shabaha ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendana na malengo ya Serikali yake ya kuinua uwezo wa kiujuzi wa vijana wa Tanzania ambao wanakadiriwa kuwa zaidi asilimia 50% ya watanzania wote.