Ubora wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan unadhihirishwa na matokeo ya wazi ya mabadilliko anayoyafanya, katika jitihada za kuboresha maisha ya watanzania.
Kupitia ziara yake mkoani Katavi, imefahamika kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameandika historia ya kuwa Rais wa kwanza tokea nchi ya Tanzania ipate uhuru, kufikisha umeme wa Gridi ya Taifa mkoani Katavi. Mkoa huo uliokuwa unapata umeme kupitia mafuta ya dizeli yaliyokuwa yanagharimu zaidi ya bilioni mbili kwa mwezi mmoja, sasa wamepata ukombozi wa uhakika utakaowawezesha kuwekeza kikamilifu kwenye miradi mbalimbali ya kimaendeleo inayohusisha nishati ya umeme.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia uwekezaji mkubwa wa fedha za kitanzania shilingi bilioni 1.4, amewezesha kufanyika kwa mageuzi makubwa katika uwanja wa ndege wa mkoa wa Katavi ambao wakati anaingia madarakani, haukuwa na barabara ya lami yenye kiwango kizuri cha kuruhusu ndege kubwa kutua. Mbali na hapo, fedha hizo zimewezesha kujengwa kwa jengo jipya la abiria, ambalo linauwezo wa kupokea abiria 400 kwa wakati mmoja, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo jengo la uwanja huo lilikuwa linaruhusu wageni 40 tu.
Historia nyingine ya kipekee ambayo imekuwa na matokeo chanya kwa wakazi na wananchi wa mkoa wa Katavi ni ununuzi wa ndege za kubebe abiria, ambao Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amefanya. Baada ya ununuzi wa ndege hizo na ukarabati mkubwa wa uwanja wa ndege wa mkoa huo, idadi ya safari za ndege za kuelekea Katavi zimeongezeka tofauti na ilivyokuwa awali. Kwa sasa, kuna safari tatu za ndege za kwenda Katavi kila wiki, tofauti na ilivyokuwa awali kabla Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, hajaingia madarakani ambapo safari za ndege kuelekea Katavi ilikuwa moja tu kwa wiki.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka historia ya aina yake ya kuufanya mkoa wa Katavi kuwa kanda maalumu ya kimkakati, kwa kuupq uwezo wa kununu mazao ya nafaka peke yake. Hatua hii imefuatia uwezo mkubwa wa uzalishaji wa mazao ya nafaka, uliopelekea Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuongeza maghala ya kisasa ya kuhifadhia chakula ambayo yatakuwa na uwezo wa kuhifadhi zaidi ya tani 8,000 za mazao ya chakula tofauti na uwezo wa awali wa kuhifadhi tani 5,000 pekee.
Upekee wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mkoa wa Katavi unajidhihirisha pia kwenye upande wa miundombinu ya barabara ambapo ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake, Rais Dkt. Samia amejenga barabara za kiwango cha lami ambazo nyingine zimekamilika na nyingine ziko mbioni kukamilika. Barabara hizo ni, barabara ya Kibaoni mpaka makutano ya Mlele (kilomita 50), Vikonge mpaka Luhafwe (kilomita 25), Luhafwe mpaka Mishamo (kilomita 37.5), Kagwira mpaka Karema (kilomita 110).
Licha ya hayo yote, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kutambua mchango sekta ya uvuvi ameahidi kuendelea kutoa mafunzo ya uvuvi wa kisasa kwa wavuvi wa mkoa wa Katavi pamoja na boti za kisasa za kuvulia samaki, huku akiahidi kulilinda Ziwa Tanganyika ili liendelee kuwa chanzo kikuu cha mapato ya mazao ya ziwa, kwa kuhimiza uvuvi salama unaozingatia utunzaji wa mazingira.
Ushahidi huu wa mkoa wa Katavi, juu ya ufanisi na uhalisia wa kimatokeo, unadhihirisha kuwa miaka mitatu ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekuwa ya mageuzi makubwa ambayo yanaacha alama itakayodumu kwa vizazi vingi vijavyo.