Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiongoza Serikali yake ya awamu ya Sita, kufanya mageuzi makubwa kwa sekta ya mifugo, na kuifanya sekta hiyo kuwa na tija kubwa kwa ustawi wa Taifa kupitia ukuaji wa mchango wake kwa pato la Taifa.
Hamasa iliyotolewa na Rais Dkt. Samia imehusisha kutoa elimu ya ufugaji wa kisasa kwa wafugaji wa hapa nchini, huku ikirahisisha uingizaji wa mbegu bora, za kisasa na muda mfupi za mifugo mbalimbali kwa madhumuni ya kuongeza tija ya kiuchumi katika ufugaji.
Serikali ya awamu ya Sita chini ya Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imetumia sera yake ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki ya diplomasia ya uchumi, kutafuta masoko ya bidhaa za mifugo zinazopatikana hapa nchini.
Msimamo wa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, juu ya mustakabali wa ufugaji na wafugaji hapa nchini, unabakia kuwa wa kuleta tija ya kiuchumi kwa wafugaji wenyewe lakini pia kwa Serikali kupitia mapato kwa Serikali.
Ili kuiweka Tanzania kwenye ramani ya mataifa yenye mifugo mingi kwa idadi na ubora, Serikali ya Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan imesimamia hatua mbalimbali za kuhakikisha kunakuwa na ongezeko la mifugo, kwa madhumuni ya kukidhi mahitaji ya masoko ya ndani na nje ya nchi.
Takwimu rasmi zilixorekodiwa na wizara ya mifugo na uvuvi, zinaonyesha matokeo chanya ya ongezeko la mifugo ya kimkakati kwa kipindi cha miaka mitatu ambayo Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameiongoza Tanzania.
Idadi ya mifugo hapa nchini imeongezeka ambapo idadi ya ng’ombe imeongezeka kutoka ng’ombe milioni 33.9 mwaka 2021 mpaka kufikia ng’ombe milioni 35.3 mwaka 2023.
Kati ya ng’ombe milioni 35.9 waliopo nchini, ng’ombe wa kisasa wa maziwa ni milioni 1.26. Shauku kubwa ya Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imekuwa ni kubadili kabisa aina ya ufugaji wa ng’ombe za maziwa, ambapo mkazo mkubwa wa Serikali ya awamu ya Sita, umkuwa ni kutoa elimu na mafunzo kwa wafugaji kubadili mifugo kutoka ya asili na kuwa na mbegu za kisasa zenye matokeo makubwa kwa uwiano wa idadi ndogo.
Uzalishaji wa maziwa nchini umeongezeka kutoka lita bilioni 3.1 mwaka 2020/21 hadi kufikia lita bilioni 3.4 mwaka 2022/23. Kutokana utafiti uliofanywa, lita bilioni 2.3 zilitokana na ng’ombe wa asili na lita bilioni 1.1 zilitokana na ng’ombe wa kisasa wa maziwa.
Kupitia diplomasia ya uchumi ya Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan iliyohamasisha uwekezaji mkubwa zaidi wa viwanda vya kusindika maziwa kutoka 99 mpaka kufikia 105, kumekuwa na ongezeko kubwa la vituo vya kukusanyia maziwa kutoka 221 hadi kufikia 238 ambavyo kwa wastani vinakusanya zaidi ya lita milioni 77.6.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya uongozi wa Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan imefanikisha kuhamasisha ongezeko la usindikaji wa maziwa kutoka lita milioni 75.9 hadi kufikia lita lita 77.6, ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 2.2. Kufanikiwa huko kumetokana na utoaji wa elimu ya ufugaji bora wa kibiashara wa ng’ombe wa maziwa.
Kwa upande wa uzalishaji wa nyama, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kipindi cha miaka mitatu, iliyoongozwa na Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeshuhudia ongezeko la tani za nyama kutoka tani 738,166 zilizozalishwa mwaka 2020/21 hadi kufikia tani 769,966.7 za mwaka 2021/22.
Ongezeko la tani za nyama limetokana na ongezeko la idadi ya mifugo hapa nchini ambapo mbali ng’ombe kuongezeka hadi kufikia milioni 35.3, mbuzi wameongezeka kutoka milioni 24.5 hadi kufikia milioni 25.6, huku kondoo wakiongezeka kutoka milioni 8.5 hadi kufikia milioni 8.8. Kuku wameongezeka kutoka 87.7 hadi milioni 92.8, ambapo kati ya hao, kuku wa asili wameingezeka kutoka milioni 40.4 hadi milioni 42.7, na kuku wa kisasa wameongezeka kutoka milioni 47.3 hadi kufikia milioni 50.1. Nguruwe katika kipindi hiki kifupi wameongezeka kutoka milioni 3.2 hadi kufikia milioni 3.4.
Ongezeko hili linatajwa kama matunda ya uwepo wa Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kama Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutokana na jitihada zake binafsi za kuwaunganisha wazalishaji wa nyama hapa nchini, na viwanda, wazalishaji na makampuni kutoka nje ili kubadilishana ujuzi na uzoefu pamoja kuanzisha makubaliano ya kushirikiana kwa malengo ya kuiimarisha sekta hiyo.