Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya kikazi mkoani Katavi kuanzia tarehe 12 mpaka 15 ya mwezi huu wa 7.
Ziara hiyo iliyotangazwa na Kurugenzi ya mawasiliano ya Ikulu, itaangazia mambo mbalimbali ikiwemo ukaguzi wa miradi mbalimbali ambayo Serikali ya awamu ya Sita (6) imeitolea mafungu ya fedha.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, pia anatarajiwa kufanya mikutano kadhaa ya hadhara ambayo italenga kuwahutubia watanzania wote kupitia wananchi wa mkoa huo wa Katavi. Kupitia mikutano hiyo, Rais. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ataendelea kutoa dira ya muelekeo wa utendaji wa Serikali yake pamoja na mrejesho wa hatua mbalimbali ambazo Serikali imezichukua katika kuinua hali za wananchi kiuchumi na huduma za kijamii.
Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa pia kutoa nafasi kwa wakazi wa mkoa wa Katavi kuelezea kero na changamoto zao kwa ajili ya kuzipatia ufumbuzi na utatuzi.
Kupitia ziara hiyo ya siku tatu, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anatarajia pia kuhamasisha wananchi wa mkoa wa Katavi kuchangamkia fursa za kiuchumi zitokanazo na mahusiano ya kidiplomasia ambayo Serikali imekuwa ikiyaweka na mataifa mengine ulimwenguni kote.
Ziara hiyo pia inatarajiwa kuwakutanisha watendaji wakuu wa mkoa huo na Mh. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambae ataitumia ziara hiyo kupima utendaji na ufanisi wa wawakilishi wake kupitia utimizaji wa malengo na maagizo ya Serikali.