Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan amehakikisha kipaumbele cha ukuzaji wa uchumi na kupunguza umasikini wa kipato kwa kaya duni, kinaendelea kuwa msingi mkuu wa uongozi wake, katika kuinua hali ya wananchi masikini nchini.
Rais Dkt. Samia ameendelea kuusimamia kikamilifu Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kuinua ubora wa maisha na ustawi wa jamii pamoja na Utawala bora na uwajibikaji.
Katika hali ya kuwajali wananchi wake, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), hadi kufikia mwezi Machi, 2024, alikua amesimamia uhakiki wa kaya katika Mamlaka 135 za utekelezaji ili kutambua hali za ustawi wa maisha ya kaya za walengwa wa Mpango huo. Jumla ya kaya 607,995 zilihakikiwa na uchakataji wa takwimu unaendelea ili kubaini kaya ambazo zimeboreka kiuchumi na zile ambazo zitaendelea kuwepo kwenye Mpango huo.
Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewasilisha ruzuku ya shilingi za kitanzania bilioni 169 kwa kaya za walengwa 1,336,600 zenye jumla ya wanakaya 5,164,333 kutoka katika maeneo 186 ya utekelezaji yanayojumuisha Tanzania bara, Unguja na Pemba kwa upande wa Zanzibar ili waweze kujikimu na mahitaji yao ya msingi.
Serikali ya awamu ya Sita ya Dkt. Samia Suluhu Hassan, ilibuni jumla ya miradi 10,442 ya ajira za muda, ambayo ilianza kutekelezwa katika maeneo ya utekelezaji 123 ambapo kaya za walengwa 609,114 zimejumuishwa kushiriki kutekeleza miradi hiyo yenye thamani ya jumla ya shilingi bilioni 105.7.
Kati ya fedha hizo, shilingi bilioni 11.6 zilitumika kwa ajili ya ununuzi wa vitendea kazi na shilingi bilioni 94.1 zilitumika kwa ajili ya ujira wa kaya za walengwa wanaofanya kazi katika miradi hiyo.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan maeiongoza Serikali yake kuibua miradi 1,037 ya kuendeleza miundombinu, ambapo utekelezaji wa miradi hiyo upo katika hatua mbalimbali ambapo, miradi 252 katika sekta za afya, elimu, ujasiriamali, barabara za vijijini, maji na mazingira imekamilika na kuanza kutoa huduma.
Rais Dkt. Samia ametumia jumla ya shilingi bilioni 65.01 katika utekelezaji wa miradi hiyo iliyojumuisha jumla ya wataalam 120 kutoka kwenye Mamlaka za utekelezaji wa mpango 25 walipatiwa mafunzo ya uwezeshaji na usimamizi wa miradi hiyo.
Hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali ya awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kusimamia uundwaji wa vikundi 6,527 vyenye wanachama 87,913 katika Mamlaka 35 za Utekelezaji ndani ya Tanzania bara.
Kupitia vikundi hivyo, jumla ya walengwa 17,931 kutoka kwenye maeneo ya utekelezaji 35, wamepewa ruzuku ya uzalishaji yenye thamani ya bilioni 1.7 ili waweze kuanzisha shughuli za kiuchumi.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imewezesha mafunzo kwa wawezeshaji 808 kuhusu uhamasishaji na uundaji wa vikundi, uwekaji wa kumbukumbu za taarifa za fedha, usimamizi wa mikopo pamoja na utatuzi wa migogoro.
Dkt. Samia Suluhu Hassan, amehakikisha kuwa walengwa 503,618 ambao ni sawa na asilimia 38 ya walengwa wote wamelipwa kwa njia ya kielekitroniki kwa malipo ya kipindi cha mwezi Septemba na Oktoba, 2023 ambapo asilimia 49 walilipwa kuoitia benki na asilimia 51 walilipwa kwa mitandao ya simu. Serikali ya awamu ya Sita, imetumia zaidi ya bilioni 18 kuwalipa walengwa hao.
Wanufaika wa mfuko huo maendeleo wa TASAF wameendelea kushuhudia ukubwa wa msukumo unaowekwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuwainua, kupitia mikakati thabiti na fedha zinazotolewa kwa wakati, kww walengwa wa kaya duni zinazotegemea kuinuliwa kichumi.