Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan amehimiza uwajibikaji na ushirikiano baina ya viongozi wa ngazi mbalimbali Serikalini ili kuboresha utendaji na kuwa na matokeo mazuri katika kuwahudumia wananchi.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameyasema hayo visiwani Zanzibar, kwenye Ikulu ndogo ya Tunguu, alipokuwa akiapisha viongozi aliowateua karibuni.
Azma ya Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona kitovu cha biashara nchini, soko la Kariakoo, linafanya kazi kwa saa 24 pindi ujenzi wa soko hilo utakapokamilika.
Maagizo mahsusi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa Waziri wa Viwanda na Biashara ni kuhakikisha anaweka ukaribu wa kikazi baina ya wizara yake na Wizara ya Mipango na Uwekezaji, huku pia akihimizwa kuifungamanisha wizara yake na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam ili kusimamia sekta ya biashara katika soko hilo kwa madhumuni ya kuimarisha ufanisi na huduma kwa wafanyabiashara.
Katika hali ya kuongeza ukaribu baina ya Serikali na wafanyabiashara, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameagiza uchukuaji wa hatua za makusudi kutengeneza mahusiano mazuri na wafanyabiashara kote nchini, pamoja na kutatua kero zao, ili kuhamasisha ongezeko la wafanyabiashara na imani yao juu ya Serikali.
Akionyesha hali ya kuwajali wafanyabiashara wazawa, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amemuelekeza waziri Jafo, kuhakikisha wizara yake inakuwa na kanzidata ya wafanyabiashara wote, pamoja na kuwa makini na utoaji wa leseni, ili kutokutoa leseni kwa wafanyabiashara kutoka nje ya Tanzania kwa kazi zinazoweza kufanyika na watanzania.
Kutokana na ukubwa wa miradi inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya Sita, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amemuagiza Kamishna Mkuu mpya wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Yusuph Mwenda, kuziba mianya ya ukwepaji wa kodi na kuongeza wigo, ubunifu na kasi ya ukusanyaji wa mapato ya ndani, ili Taifa liondokane na mikopo kutoka nje.
Kupitia hadhara hiyo, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amemtaka Kamishna Mwenda, kuhakikisha mifumo ya TEHAMA kati ya TRA na na Mamlaka ya Bandari inasomana ili kuweza kukusanya kodi itakayosaidia kuwekeza kwenye miradi ya kimkakati ya maendeleo, pamoja na kuhakikisha wafanyabiashara wote nchini wanatumia mashine za kielektroniki (EFD), huku pia akitoa rai kwa wananchi kudai risiti kutokana na matumizi wanayofanya ili kuweka hali ya uwajibikaji kwa wafanyabiashara.