Serikali ya awamu ya Sita, ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kutekeleza majukumu yake, kupitia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), ya kuchukua hatua stahiki za kuzuia na kupambana na rushwa.
Hatua ambazo Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imezichukua ni pamoja na kuzuia na kupambana na rushwa kwenye sekta ya umma, mashirika na sekta binafsi, kuchunguza tuhuma za makosa ya rushwa, kuwafikisha watuhumiwa wa tuhuma za makosa ya rushwa, kuwafikisha watuhumiwa wa tuhuma za rushwa na ufisadi mahakamani pamoja na kuwekeza kwenye kutoa elimu kwa umma juu ya madhara ya rushwa.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea kuwa mpambanaji namba moja dhidi ya rushwa kwa yeye mwenyewe kuongoza mapambano ya kutokomeza vitendo vya rushwa nchini, kwa kuiwezesha Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini, kwa nyenzo muhimu za kuwawezesha kutekeleza kazi zao, kama rasilimali fedha, na miundombinu mingine wezeshi.
Katika kipindi chake kifupi, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, alielekeza ufuatiliaji na uchunguzi wa miradi ya maendeleo 1,086 yenye thamani ya Shilingi bilioni 743.90, ambapo miradi 179 yenye thamani ya Shilingi bilioni 61.01 ilibainika kuwa na kasoro mbalimbali ambazo zilipelekea uchukuaji wa hatua stahiki.
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan pia aliongoza kwa kuelekeza na kusimamia uchambuzi wa mifumo 446 kwa lengo la kubaini mianya ya rushwa katika maeneo ya huduma za jamii, fedha majengo, utawala, usafirishaji, biashara, umeme, kilimo na misitu.
Rais Dkt. Samia katika mapambano yake, ameshuhudia jumla ya kesi 767 zikiendeshwa mahakamani zikiwemo kesi mpya 314.
Kati ya kesi mpya zilizofunguliwa mahakamani, tatu (3) ni kesi ambazo kila moja thamani yake inaanzia shilingi bilioni 1 na kuendelea, ambazo zilifunguliwa katika Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.
Kesi 259 ziliamuliwa mahakamani ambapo Jamhuri ilishinda kesi 175 kwa watuhumiwa kuhukumiwa kifungo au/na kulipa faini. Katika jitihada hizo hizo, hadi kufikia mwezi Machi, 2024, kesi 453 zilikuwa zinaendelea mahakamani.
Kutokana na jitihada hizi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kiasi cha shilingi bilioni 15.40 zimeokolewa kutokana na operesheni mbalimbali za uchunguzi uliofanyika kote nchini ambapo shilingi bilioni 14.46 ni fedha taslimu zilizorejeshwa Serikalini huku bilioni 1.04 zikidhibitiwa.
Katika hatua nyingine, Serikali ya awamu ya Sita, chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, mchakato wa marekebisho ya Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 unaendelea na maoni kutoka kwa wadau yamekusanywa.
Katika hatua ya kuhakikisha kizazi kijacho kinaandaliwa vyema kudhibiti vitendo vya rushwa kwa ustawi wa Taifa kwa miaka mingi ijayo, Serikali ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imehusika kikamilifu katika uanzishwaji wa klabu za wapinga rushwa 128 katika shule za msingi na sekondari.
Zaidi ya hapo, klabu za wapinga rushwa 4,797 zilizokuwepo awali, ziliimarishwa na TAKUKURU imeendelea kuelimisha vijana wa SKAUTI ili kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kupitia kazi.
Kupitia hatua hizi na nyingine nyingi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anaendelea kujipambanua kama mpinga rushwa namba moja, mwenye imani na uthabiti wa kutokomeza rushwa nchini.