728 x 90

Diplomasia ya Uchumi ya Rais Samia yamkosha Rais Nyusi wa Msumbiji.

  • July 3, 2024
Diplomasia ya Uchumi ya Rais Samia yamkosha Rais Nyusi wa Msumbiji.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kung’ara kutokana na ukomavu wake wa kisiasa, kupitia sera anazoziamini na kuzitumia kuleta mabadiliko ya kimtazamo katika kuinua uwezo wa Taifa kiuchumi kupitia falsafa ya diplomasia ya uchumi.

Kupitia taarifa iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu, Rais wa Msumbiji, Mh. Filioe Jacinto Nyusi ameonyesha na kuelezea uwezo wa Rais Samia kumudu kuongoza mageuzi ya nchi yake yenye athari chanya mpaka kwa nchi jirani.

Akielezea umuhimu wa miundombinu kwa ukanda huu wa nchi za kusini mwa Jangwa la Sahara, Rais Nyusi ameonyesha shauku kubwa juu ya miradi ya kimkakati inayotekelezwa na Serikali ya awamu ya Sita ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Rais Nyusi ametamka kuwa mahitaji ya nishati katika ukanda huu, kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya ukuaji wa uchumi unaotegemea viwanda, utasaidika sana kupitia umeme utakaozalishwa katika bwawa la Mwalimu Nyerere.

Rais Nyusi ameiona pia fursa kubwa ya uwezo wa kusafirisha bidhaa na mazao nje ya nchi kupitia mradi wa treni ya umeme ambao unatajwa kama fursa kwa wafanyabiashara wa mataifa jirani kutokana na kupunguza gharama huku ikiwahisha mahitaji kwa usalama zaidi.

Kupitia kikao cha Marais hao, Rais Nyusi amewapongeza watanzania kwa kuwa na kiongozi shujaa aina ya Dkt. Samia, ambae kupitia maelekezo na mikakati yake, amani na utulivu umerudi katika mpaka wa Tanzania na Msumbiji ambao kwa kipindi kirefu ulikua na hali ya kukosa utulivu, hali iliyopelekea hasara kwa mataifa hayo mawili kutokana na kuzorota kwa biashara kupitia mpaka huo.

Aidha, Rais Nyusi wa Msumbiji ametumia mkutano huo kusifu jitihada za Tanzania kuhamasisha na kutekeleza uchumi wa buluu na kulisuka upya shirika la ndege la Tanzania (ATCL). Nchi hizo mbili zimekubalia kushirikiana kuinua uchumi wa buluu kwa pamoja, huku zikiazimia uanzishwaji wa safari za anga kati ya Tanzania na Msumbiji.

Katika kuimarisha ushirikiano baina ya Tanzania na Msumbiji, viongozi wa nchi hizo wameshuhudia utiaji saini wa makubaliano katika sekta ya afya inayolenga kufanya tafiti, kubadilishana uzoefu na kufanya programu za pamoja baina ya Tanzania na Msumbiji.

Mbali na hapo, Marais hao pia walishuhudia utiaji saini wa makubaliano kati ya Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Taasisi ya Uwekezaji na Uwezeshaji ya Msumbiji yanayolenga kuimarisha ushirikiano na kupanua mawanda ya biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Msumbiji.

Sera ya Diplomasia ya Uchumi inayoongoza mahusiano ya Tanzania na mataifa mengine na washirika wengine wa kimataifa, ndiyo imepelekea Rais wa Msumbiji, Mh. Filipe Nyusi kupewa heshima ya kuyafungua rasmi maonyesho makubwa ya kibiashara nchini Tanzania ya sabasaba, kama sehemu ya kutangaza fursa mbalimbali za kibiashara zinazopatikana Tanzania kwa wafanyabiashara kutoka Msumbiji.

Diplomasia ya Uchumi inayoangazia kuzifungua sekta mbalimbali nchini kwa wawekezaji na wabia wa nje, ndiyo inayompeleka Rais Nyusi wa Msumbiji, Visiwani Zanzibar kwa ajili ya kujionea zaidi ufanisi wa uchumi wa buluu na utalii.

Katika hali ya kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa wananchi wa Tanzania na Msumbiji, nchi hizo zimekubaliana kuanzisha umoja wa wazalishaji wa korosho, kama sehemu ya kurasimisha kilimo hiko, kwa kukiongezea thamani na tija, hali itakayobadili uhudumiaji wa zao hilo na kupandisha bei ya zao hilo.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amekuwa na muendelezo wa kasi, wenye matokeo mazuri wa sera yake ya Diplomasia ya Uchumi inayolenga kuvuna ushirikiano wa mataifa mengine katika kutimiza malengo ya Tanzania katika kujiletea maendeleo.