728 x 90

Ziara ya Rais Nyusi nchini ni matokeo ya Diplomasia ya Uchumi nchini chini ya Dkt. Samia Suluhu.

  • July 2, 2024
Ziara ya Rais Nyusi nchini ni matokeo ya Diplomasia ya Uchumi nchini chini ya Dkt. Samia Suluhu.

Ujio wa Rais wa Msumbiji Mh. Felipe Jacinto Nyusi hapa nchini ni kiashiria kingine cha ufanisi wa mpango kazi wa Tanzania katika kushirikiana na mataifa mengine kisiasa, kiuchumi, kijamii na nyanja nyingine mbalimbali zenye tija na maslahi kwa Taifa.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea na kasi yake ya kuitumia diplomasia ya uchumi kuendelea kufungua fursa mbalimbali nchini kwa kufungua milango kwa wawekezaji wenye maono na tija lakini vilevile kuwawezesha watanzania kuyafikia masoko ya nje, kwa kusaini mikataba na kuingia makubaliano ya ushirika wa aina hiyo.

Mkakati wa Rais Dkt. Samia ni kukuza biashara kati ya Tanzania na mataifa yanayoendelea kama mojawapo ya mkakati wa kukuza uchumi wa nchi zinazotambulika kama zinazoendelea. Ujio wa Rais Filipe Nyusi utaangazia nyanja mbalimbali za kilimo, madini, utalii mafuta na gesi.

Kupitia taarifa rasmi ya Wizara ya Mambo ya Nje, ilielezwa kuwa Rais Nyusi amepewa heshima ya kufungua maonyesho rasmi ya biashara nchini, ambayo maana yake ni kukaribisha watu wa nchi ya Msumbiji kuwa sehemu ya maonyesho hayo ambayo inatazamiwa itaongeza washiriki na mzunguko mkubwa zaidi wa biashara itakayofanyika.

Ziara hii inakuwa sehemu ya muendelezo wa jitihada za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuifanya Tanzania kuwa kitovu cha biashara baina ya nchi za Afrika, hasa baada ya ziara ya Rais wa Guinea-Bissau, Mh. Umaro Sissoco Embalo kumalizika karibuni.

Tanzania inatajwa kuwa na mvuto wa kipekee kibiashara kwa mataifa mengine kutokana na utajiri wa rasilimali ambao unatoa fursa za kipekee za ushirikiano kwa ajili ya manufaa ya watanzania na wawekezaji kutoka nje.

Katika hatua nyingine, ziara hii ya Rais Nyusi inakuwa ziara yake ya mwisho nchini kama kiongizi wa taifa lake kutokana na muda wake wa kuiongoza nchi hiyo kikatiba kutamatika. Kutokana na uhusiano uliodumu kuanzia zama za kupigania uhuru zilizoongozwa na waasisi wa mataifa haya, Mwl. Julius K. Nyerere kwa upande wa Tanzania na Eduardo Chivambo Mondlane, Rais Nyusi ameipa Tanzania heshima ya kipekee ya kuja kuiga rasmi, kitendo kinachotafsiriwa kama kudumisha ukaribu wa miaka mingi.