728 x 90

Diplomasia ya Uchumi ya Rais Samia yaleta tija kwa kilimo cha Tanzania.

  • July 1, 2024
Diplomasia ya Uchumi ya Rais Samia yaleta tija kwa kilimo cha Tanzania.

Hakuna nchi katika historia ya ulimwengu iliyowahi ama kujitegemea au kujitosheleza kwa mahitaji yake.

Hivyo, nyenzo ya ushirikiano ni muhimu kwa mataifa yote ili kuhakikisha mahitaji ya msingi ya watu wake yanatimizwa hata ikibidi kwa kutumia rasilimali zinazopatikana nje ya nchi husika.

Mkakati mkubwa wa Tanzania katika kutimiza malengo iliyojiwekea ni diplomasia ya uchumi. Mkakati huu huusisha matumizi ya ushiriki chanya, ujirani mwema, utunzaji wa urafiki mzuri, ustaarabu na kuheshimu taratibu, mila, miiko ya nchi nyingine ili kujenga imani ushirikiano wa pamoja katika kufanya biashara za nchi kwa nchi.

Aina hii ya diplomasia ina asilimia kubwa ya kuisaidia nchi inayoamua kuitumia, mafanikio na faida za kimkakati kwa ajili ya ustawi wa watu wake na ukuaji wa uchumi kiujumla.

Tanzania imetangaza karibuni kuuza zaidi ya tani za mahindi 650,000 kwa Taifa la Zambia ambalo limepitia changamoto ya ukame wa muda mrefu. Hii kwa ufupi wake ni faida mojawapo itokanayo na matumizi ya diplomasia ya uchumi.

Mkataba huo unaotarajiwa kutekelezwa kwenye kipindi cha miezi nane, unatarajiwa kuiingizia Tanzania kiasi cha shilingi za kitanzania 650 bilioni, ambayo itatumika kuinua sekta ya kilimo nchini kwa kuwawezesha wakulima kumudu kununua vifaa vya kisasa na kuwapa uwezo wa kulima kwenye maeneo makubwa zaidi.

Mkataba huo unaohusisha kutoa mazao hayo katika maghala ya Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ulisainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa NFRA, Dkt. Andrew Komba kwa upande wa Tanzania pamoja na Mratibu wa Maafa kitaifa nchini Zambia Dkt. Gabriel Pollen.

Hii ni hatua muhimu iliyofikiwa kupitia uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizi mbili, unaozaa matunda mema ya faida ya kiuchumi kwa Tanzania na uhakika wa chakula kwa Zambia.

Mafanikio haya makubwa kwa upande wa Tanzania yamekuja kutokana na uwezo mkubwa wa kuona mbali na wa kutafsiri maono na ndoto, alionao Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Rais Samia ameinua sekta ya kilimo iliyokuwa imedorora kwa miaka mingi kwa kuongeza bajeti ya wizara ya kilimo, kuondoa ushuru wa forodha kwa vifaa muhimu ya kilimo, kugawa mbolea kwa bei nafuu na kutafutia wakulima masoko ya nje ya nchi.

Yote haya yanawezekana kutokana na utekelezaji wa sera ya diplomasia ya uchumi inayoipa Tanzania kupitia Rais wake Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, taswira njema ya ukarimu, wema na urafiki wa kweli katika hali zote.

Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa kiongozi anaeaminika barani Afrika na kwingineko duniani kutokana na utashi wake unaoendana na marais waliotangulia, walioijengea Tanzania heshima katika siasa za kimataifa.

Diplomasia ya uchumi imayofanywa na Rais Samia inagusa sekta zote ikiwemo utalii, viwanda, usafiri, madini, elimu, na nyingine nyingi.

Wakati mataifa mengine yakichagua aina nyinginezo za kutimiza malengo yao katika mahusiano na mataifa mengine, mkataba huu wa mauziano ya mahindi kati ya Tanzania na Zambia yanatoa uthibitisho wa usahihi wa njia anazopita Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha anabadilisha hali za watanzania kwa kuinua uchumi wao.