728 x 90

Serikali kuwainua wanawake kwa kuwapa mashine za kubangua korosho.

  • June 28, 2024
Serikali kuwainua wanawake kwa kuwapa mashine za kubangua korosho.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imekusudia kuwainua wanawake nchini kwa kudhamiria kutoa mashine za kubangua korosho kwa vikundi vya wanawake, ili kuwainua kiuchumi kwa kuwawezesha kuongeza thamani ya bidhaa zao.

Kauli hiyo imetamkwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Kilimo, Mh. David Silinde alipokuwa akijibu swali la mbunge wa viti maalum, Mh. Agnes Elias Hokororo aliyetaka kujua, Serikali ina mpango gani kupitia SIDO kutoa mashine za ndogo za na rahisi kwa vikundi vya wanawake vya ubanguaji wa korosho Mkoani Mtwara.

Naibu Waziri, Mh. Silinde ameliambia Bunge kuwa, Serikali katika mwaka wa fedha 2023/24 kupitia Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO) imeendelea kushirikiana na wadau wengine katika tasnia ya korosho kuwezesha utengenezaji na usambazaji wa mashine ndogo za kubangulia korosho kwa vikundi vya vijana na wanawake.

Akielezea maendeleo yaliyopatikana hadi kufikia mwezi Aprili, 2024, Mh. David Silinde amesema jumla ya mashine 100 zenye uwezo wa kubangua kilo 8-12 kwa siku zimenunuliwa na kusambazwa kwenye vikundi vya ubanguaji katika Mikoa inayozalisha Korosho. Kati ya hizo, Mh. Silinde amesema, mashine 71 zimesambazwa kwenye vikundi 15 vya vijana na wanawake wanaojishughulisha na ubanguaji wa korosho mkoani Mtwari.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mh. Silinde, ameliambia Bunge kuwa, Bodi ya Korosho Tanzania kwa kushirikiana na NMB Foundation wametoa mafunzo kwa wabanguaji wa korosho 537 wakiwemo wanaume 160 na wanawake 377 kutoka wilaya za Newala, Tandahimba, Nachingwea na Ruangwa.

Mh. David Silinde, amesema Serikali ya awamu ya Sita imeendelea na zoezi la kutoa mafunzo kwa wabanguaji kwa wilaya zote zinazozalisha zao la korosho hapa nchini.