Naibu Waziri wa Kilimo, Mh. David Silinde ameyasema hayo alipokuwa anajibu swali lililoulizwa na mbunge wa jimbo la Mbozi aliyeuliza ni lini Serikali itawachukulia hatua viongozi wa vyama vya msingi waliodhulumu fedha za wakulima wa kahawa Mbozi.
Mh. Silinde amelieleza Bunge kuwa, tayari Serikali imeshafanya uchunguzi kwa vyama vya ushirika 20 vilivyopo wilayani Mbozi ambapo kati ya hivyo, vyama nane (8) vimekutwa na changamoto mbalimbali ikiwemo wakulima kupunjwa malipo ya mauzo ya kahawa, na baadhi ya kampuni za ununuzi wa kahawa kushindwa kulipa fedha za mauzo ya kahawa kwa Chama cha Ushirika.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa baada ya uchunguzi, Naibu Waziri, Mh. Silinde amelidokeza Bunge kuwa, Serikali kupitia Tume ya Maendeleo ya Ushirika imekamilisha mapitio ya taarifa hizo na kuanza kuchukua hatua stahiki kwa viongozi na watendaji waliobainika kuhusika na ubadhilifu uliojitokeza.
Mh. Silinde alizitaja baadhi ya hatua zilizochukuliwa kuwa ni pamoja na viongozi wa vyama vya ushirika kuondolewa kwenye uongozi na kufunguliwa kesi katika Mahakama ya Hakimu Mfawidhi wa Mkoa wa Songwe.