728 x 90

Serikali yaboresha maslahi ya askari wa uhamiaji.

  • June 28, 2024
Serikali yaboresha maslahi ya askari wa uhamiaji.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongizwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendeleza kasi yake ya kuboresha maslahi ya askari wa idara ya uhamiaji nchini, kama sehemu ya motisha ya kazi nzuri inayofanywa na askari wa idara hiyo muhimu kwa usalama wa nchi yetu.

Kauli hiyo imetamkwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mh. Daniel Baran Sillo Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu swali la mbunge wa viti maalum, Mh. Tunza Issa Malapo, alieomba ufafanuzi wa Serikali juu ya ni lini itaboresha maslahi ya askari wa idara ya uhimiaji nchini.

Kupitia majibu yake, Naibu Waziri, Mh. Sillo aliliambia Bunge kuwa, Serikali imeendelea kuboresha maslahi ya maafisa, wakaguzi na askari wa idara ya uhamiaji kadiri hali ya fedha inavyoruhusu.

Naibu Waziri, Mh. Sillo alilitaarifu Bunge kuwa, kwa mwaka wa fedha 2023/24 Serikali iliridhia posho mbalimbali ambazo ni posho ya chakula, nyumba, ujuzi na utaalamu.

Naibu Waziri Mh. Sillo alitoa taarifa kwa Bunge kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25 Serikali imeongeza posho ya upelelezi, madaraka, intelijensia na ukufunzi.

Katika kuhitimisha majibu ya Serikali kwa swali la Mh. Malapo, Naibu Waziri, Mh. Sillo aliliambia Bunge kuwa Idara ya Uhamiaji imeendelea kuongeza nyumba za makazi za watumishi ambapo hadi sasa ina majengo 465 yanayokaliwa na familia 465.