Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetaja mikakati mbalimbali inayolenga kutokomeza ukatili dhidi ya watoto hapa nchini.
Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mh. Mwanaidi Khamis ameyasema hayo alipokuwa akijibu swali la mbunge wa jimbo la Wingwi, Mh. Omaari Issa Kombo aliyetaka kufahamu Serikali ina mikakati gani ya kukabiliana na vitendo vya ukatili ikiwemo mauaji yanayotokea kwenye jamii kwa sababu ya wivu kimapenzi.
Moja ya mikakati inayolenga kutokomeza ukatili wa kijinsia iliyotajwa na Naibu Waziri, Mh. Mwanaidi ni kuboresha vituo vya huduma kwa wateja ili kuwawezesha wananchi kupata elimu na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili kwa wakati.
Naibu Waziri Mh. Mwanaidi aliliambia Bunge kuwa hatua nyingine ya Serikali inayolenga kuzuia ukatili wa kijinsia ni kuendelea kutoa huduma za afya ya akili na msaada wa kisaikolojia kwa jamii na kutoa hifadhi ya dharura kwa manusura wa vitendo vya ukatili.
Naibu Waziri wa wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi, Mh. Mwanaidi Khamis ameongeza kuwa hatua nyingine iliyochukuliwa ni kuimarisha uendeshaji, usimamizi na uratibu wa mabaraza ya usuluhishi wa migogoro ya ndoa.
Kupitia majibu yake ya swali hiyo, Naibu Waziri, Mh. Mwanaidi amelibainishia Bunge kuwa mikakati hiyo imeainishwa katika Mpango wa Kazi wa Taifa wa Pili wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto pamoja na Sera ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake ya Mwaka 2023 kwa lengo la kukabiliana na vitendo vya ukatili ikiwemo mauaji yanayotokea kwenye kwenye jamii kwa sababu za wivu wa kimapenzi.