728 x 90

Serikali yatatua mgogoro kati ya hifadhi na vijiji jirani – Wanging’ombe.

  • June 27, 2024
Serikali yatatua mgogoro kati ya hifadhi na vijiji jirani – Wanging’ombe.

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imefanikiwa kumaliza mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Mpanga Kipengele na Vijiji vya Luduga, Mpanga, Malingali na Wangamiko.

Hayo yamesemwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mh. Dunstan Kitandula, alipokuwa akijibu swali la mbunge wa viti maalum, Mh. Neema William Mgaya, aliyeuliza ni lini Serikali itamaliza mgogoro wa mpaka kati ya Hifadhi ya Mpanga Kipengele na Vijiji vya Luduga, Mpanga, Malangali na Wangamiko.

Naibu Waziri, Mh. Kitandula amelieza Bunge kuwa mgogoro huo umetatuliwa baada ya kutekeleza maelekezo ya Serikali yaliyotolewa kupitia Kamati ya Mawaziri nane wa kisekta, ambayo yalihusisha kutoa sehemu ya ardhi ya Hifadhi hiyo kwa vijiji, kufyeka na kuweka alama za mpaka.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mh. Kitandula alilifahamisha Bunge kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Ofisi ya Kamishna wa Ardhi mikoa ya Njombe na Mbeya ilifanya mapitio ya mpaka wa Hifadhi ya Mpanga Kipengele na kumega eneo lenye ukubwa wa ekari 18,221.43 na eneo hilo kutolewa kwa wananchi wa vijijini vya Luduga, Mpanga, Malangali na Wangamiko.

Aidha, Mh. Kitandula ameliarifu Bunge kuwa hifadhi ya Mpanga Kipengele kwa ujumla imemega ardhi yenye ukubwa wa ekari 52,877.602 na kutolewa kwa vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo na hivyo kumaliza migogoro iliyokuwepo kati ya hifadhi na vijiji hivyo.