728 x 90

“Watu Wachache Wameshika Biashara ya Sukari ni Hatari, Serikali Ibadilishe Sheria Kunusuru Wananchi.” – Musukuma.

  • June 19, 2024
“Watu Wachache Wameshika Biashara ya Sukari ni Hatari, Serikali Ibadilishe Sheria Kunusuru Wananchi.” – Musukuma.

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Musukuma, leo ametoa mchango wake Bungeni huku akisifu hatua za Serikali kupitia Wizara ya Kilimo kutaka kubadili Sheria ya Sukari. Musukuma amesema moja ya kazi kuu za Bunge ni kutunga na kubadilisha sheria, hivyo ni muda muafaka sasa kwa serikali kufanya mabadiliko kwenye Sheria ya Sukari kwani tatizo la sukari nchini limekuwa likijirudia mara kwa mara licha ya jitihada nyingi za serikali kuleta unafuu wa bidhaa hiyo.

Mheshimiwa Musukuma alikumbusha kuwa mwaka 2019, tatizo la sukari lilikuwa kubwa sana nchini kiasi cha serikali kuingilia kati na kuvamia mabwalo ya waingizaji wa sukari nchini, hata kufikia hatua ya kutoa sukari kwa Wananchi kwa mtutu wa bunduki.

Ameongeza kuwa biashara ya sukari inashikiliwa na ‘Cartels’ (genge la wachache, mara nyingi matajiri). Mfano, Musukuma anakiri kwamba yeye kama mkaazi wa Mwanza, kipindi kilichopita cha uhaba wa sukari jijini Mwanza, sukari ilikuwa inauzwa na mtu mmoja tu, jambo ambalo ni hatari.

Musukuma amesema baadhi ya viwanda nchini vinadai kuwa na mawakala wa kusambaza sukari, lakini ukweli ni kwamba mawakala wengi ni ‘bosheni’ tu, hawana sukari.

“Kwa mfano kule Kanda za Ziwa tunakoishi sisi, watu walianza kwenda kupanga foleni saa 9 usiku kununua sukari, na huyo agent aliyetajwa hapa VH Share ambaye alikuwa wakala wa sukari, alikuwa na sukari nyingi sana ameficha kwenye maghala yake. Lakini ili uuziwe sukari, lazima ununue sukari pamoja na toilet paper au biskuti. Sasa hii ni nchi ya kistaarabu hatuwezi kuishi hivi”, amesema Musukuma.

Musukuma ameongeza kuwa ni lazima sasa serikali ibadilishe Sheria ya Sukari kunusuru wananchi. Licha ya serikali kutoa misamaha mingi na kuweka mazingira wezeshi ya kuzalisha sukari kwa wingi na kupunguza gharama ya bidhaa hiyo, bado kila mwaka hali inajirudia na kuwaweka wananchi kwenye matatizo.

Musukuma anakiri kwamba miezi michache nyuma wakati wa mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhani, wananchi wa jimbo lake walinunua sukari kwa Tsh. 11,000/- kwa kilo.

Musukuma amesisitiza kwamba ni muhimu serikali ipeleke mabadiliko ya Sheria ya Sukari Bungeni ili kutoa nafuu ya maisha kwa Watanzania na kupunguza uharamia na magenge machache ya wauzaji wa sukari nchini.