Taarifa iliyotolewa mchana wa leo na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Ikulu juu ya ziara ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhudhuria uapisho wa Rais wa Afrika Kusini Mh. Cyril Ramaphosa, utakaofanyika tarehe 19 Juni 2024, inatajwa kama sehemu ya kudumisha uhusiano wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili.
Historia ya mahusiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini ilianzia katika harakati za kupigania uhuru kutoka kwa wakoloni. Tokea kipindi hicho, nchi hizo mbili zimekuwa na ukaribu unaochagizwa na shughuli za kiuchumi, maendeleo ya huduma za kijamii, ushirika katika kupanua matumizi ya lugha ya Kiswahili, ushirikiano katika nyanja ya ulinzi na usalama, na mwingiliano baina ya wananchi wa nchi hizo kwa madhumuni mbalimbali ikiwemo mahusiano ya kibiashara na mengine ya kijamii.
Kuna umuhimu mkubwa sana na faida lukuki kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwepo katika hafla hiyo ya uapisho wa Rais Ramaphosa. Uwepo wa Dkt. Samia Suluhu Hassan utatoa ishara muhimu ya uungwaji mkono wa serikali itakayoongozwa na Rais Ramaphosa na serikali ya Tanzania.
Mbali na hapo, ushiriki wa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika sherehe za uapisho wa Mh. Ramaphosa utakuwa ni muendelezo wa ushirika unaohusisha sekta mbalimbali za kimaendeleo baina ya mataifa hayo.
Harakati jumuishi zinazohusisha mikakati ya pamoja ya kukabiliana na changamoto za pamoja kama ustawi wa kiuchumi, athari za mabadiliko ya tabianchi, kuendeleza sekta ya mifugo, na kukabiliana na janga la wahamiaji haramu zitapata nguvu mpya kutokana na ushiriki wa Rais Dkt. Samia katika sherehe za kumuapisha Rais Ramaphosa.
Ushiriki wa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika hafla itakayohudhuriwa na viongozi wa mataifa mengine utatoa nafasi ya mazungumzo kati ya viongozi hao, wanaotarajiwa kuzungumzia ustawi wa Jumuiya ya Nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara (SADC).
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia ziara hii, anauthibitishia ulimwengu mzima juu ya ushiriki chanya wa Tanzania katika siasa za kimataifa zinazoangazia zaidi ushirikiano wenye tija ya kudumisha amani, na kuongeza kasi ya ushirikiano wenye lengo la kupunguza umaskini kwa watu wa Tanzania na Afrika Kusini.
Kwa Watanzania, ziara hii ya Dkt. Samia Suluhu Hassan nchini Afrika Kusini inaendeleza chimbuko lililoasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwl. Julius K. Nyerere na Hayati Nelson Mandela la ushirikiano wa mataifa haya mawili katika hali zote.