728 x 90

Mwigulu: Asilimia 92 ya madeni ya wazabuni na wakandarasi yamelipwa.

  • June 10, 2024
Mwigulu: Asilimia 92 ya madeni ya wazabuni na wakandarasi yamelipwa.

Waziri wa fedha Mh. Dkt. Mwigulu Nchemba ameeleza kuwa Serikali ya awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeshahakiki na kulipa madeni ya wazabuni wa bidhaa na huduma pamoja na wakandarasi.

Akitolea ufafanuzi jambo hilo, Waziri wa fedha alibainisha kuwa, kufikia Machi 2024, Serikali ilikuwa inadaiwa jumla ya shilingi bilioni 1,033.01 ya madeni yaliyohakikiwa ya wakandarasi na wazabuni mbalimbali wa huduma na bidhaa.

Waziri Mwigulu, aliendelea kuelezea kuwa kati ya kiasi hiko shilingi bilioni 1,024.26 ni madeni ya wazabuni wa huduma na bidhaa huku bilioni 8.75 ni madeni ya wakandarasi mbalimbali.

Kufikia mwezi Machi mwaka huu, kwa mujibu wa waziri wa fedha, Serikali imeshalipa jumla ya shilingi bilioni 943.31 sawa asilimia 92 ya madeni yalioyohakikiwa.

Akiongeza zaidi, waziri wa fedha Mh. Dkt. Mwigulu Nchemba alidokeza kuwa, kufikia Machi 2024, Serikali ilikuwa inadaiwa jumla ya shilingi bilioni 80.06 ya madeni yaliyohakikiwa yanayotokana na kodi (VAT Refunds Claims).

Waziri Dkt. Mwigulu akaendelea kufafanua kuwa Hadi Machi 2024, Serikali imeshafanya marejesho ya jumla ya shilingi bilioni 675.1 sawa na asilimia 96 ya lengo kwa kipindi hicho.

Waziri wa fedha, Mh. Dkt. Mwigulu Nchemba ameyasema hayo bungeni Dodoma alipokuwa akijibu swali lililoelekezwa kwenye wizara yake na mbunge wa Masasi, mh Geoffrey Mwambe aliyetaka kufahamu ni kiasi gani hadi sasa Serikali inadaiwa na wazabuni, wafanyabiashara, wakandarasi na walipakodi kutokana na huduma, kazi na kodi zilizozidi.