Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Korea zimeingia makubaliano na kusaini mkataba wa mkopo wa masharti nafuu wa Dola za Marekani milioni 163.6 sawa na Tsh 427.8bn/- kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Binguni, iliyopo Zanzibar pamoja na kituo cha mafunzo ya utabibu.
Mkataba wa mkopo huo umesainiwa jijini Soeul Juni 05, 2024. Upande wa Tanzania uliwakilishwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba kwa niaba ya Serikali ya Tanzania huku Jamhuri ya Korea ikiwakilishwa na Mkurugenzi Mtendaji Mwandamizi na Mjumbe wa Bodi wa Benki ya Exim ya Korea, Hwang Kiyeon.
Ujenzi wa Hospitali hiyo utahusisha majengo ya Hospitali yenye vitengo vinne vya magonjwa Maalum kama ya kina mama na watoto, Kituo cha Mafumzo, nyumba za makazi kwa wafanyakazi, ununuzi na ufungaji wa vifaa vya matibabu vya teknolojia ya kisasa na usimikaji wa mfumo wa afya wa mawasiliano.