728 x 90

Ziara ya Dkt. Samia Korea ilivyomulika sekta nyeti ya madini na faida kwa Watanzania.

  • June 4, 2024
Ziara ya Dkt. Samia Korea ilivyomulika sekta nyeti ya madini na faida kwa Watanzania.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ameendelea kudhihirisha ushawishi wake mkubwa kwenye anga za kimataifa, baada ya kufanikiwa kuingia makubaliano maalum na Rais wa Jamhuri ya Korea Yoon Suk Yeol juu ya ushirikiano kwenye usambazaji wa madini ya kimkakati.

Makubaliano hayo yanalenga kugusa nyanja za utafiti, uwekezaji, uchimbaji na kuijengea uwezo Tanzania wa kuyaongeza thamani madini ya kimkakati yakiwemo Lithium na Nickel.

Akielezea matumaini yake, Dkt. Samia Suluhu Hassan alinukuliwa akisema “Natarajia kampuni nyingi zaidi za Korea zitashiriki katika miradi ya maendeleo inayolenga kuboresha maendeleo ya uchumi wa Tanzania na hali ya maisha kwa wakazi wake”.

Katika ujumbe wake, Rais wa Korea Kusini Yoon Suk Yeol alielezea kuvutiwa na uhusiano thabiti wa kidiplomasia baina ya nchi hizo mbili ambao umeifanya Tanzania kuwa nchi ya kwanza kutoka barani Afrika kuingia makubaliano ya kimkakati na Korea Kusini.

Nchi za Tanzania na Korea Kusini zimekusudia kuongeza ushirikaino katika sekta za nishati ya gesi asilia, filamu na sanaa. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mwenyeji wake Yoon Suk Yeol wa Korea Kusini wamekubaliana juu ya kufunguliwa kwa soko la ajira la Korea Kusini kwa vijana wa kitanzania kupitia mpango wa Employment Permit System (EPS).