Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan ametunukiwa shahada ya heshima ya udaktari nchini Korea. Shahada hiyo ni sehemu ya kutambua mchango mkubwa wakuiinua sekta ya anga nchini Tanzania ulifanywa na Dkt. Samia suluhu Hassan. Rais Samia amepongezwa kwa kazi kubwa iliyotukuka anayoifanya tokea aliposhika hatamu ya uongozi wa taifa la Tanzania. Akiwa katika chuo cha mafunzo ya anga jijini Seoul, Rais Dkt. Samia alipokea pongezi kutoka kwa rais wa chuo hicho Mh. Heo Hui-yeong.
Katika salamu zake, Mh. Heo-Hui-yeong aliuangazia mchango mkubwa wa rais Dkt. Samia kwenye kuchochea maendeleo kwa kuweka mazingira rafiki yanayovutia wawekezaji wa kimataifa. Mh. Heo Hui-yeong aliongeza kuwa rais Samia Suluhu Hassan amethibitisha kuwa ni kiongozi mwenye maono na uthubutu wa kufanya mageuzi.
Mh. Heo Hui-yeong amegusia kuwa, licha ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa Rais pekee mwanamke Barani Afrika kwasasa, hilo halijamzuia kuonyesha ukomavu wake kisiasa na ubora wa utendaji kazi katika uongozi wa nchi yake na mchango wake kwa jumuiya mbalimbali za kikanda na kimataifa.
Akiangazia sekta ya anga, mh. Heo Hui-yeong ameonyesha kustaajabishwa na uwekezaji mkubwa uliofanywa na serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan ndani ya muda mfupi. Baadhi ya mambo kama ujenzi wa viwanja vipya vya ndege, uboreshaji wa miundombinu ya viwanja vya zamani, ununuzi wa rada za kisasa pamoja na ununuzi wa ndege za kisasa za abiria na mzigo umeibadili taswira ya Tanzania katika sekta ya usafirishaji wa anga.
Katika maelezo yake mh. Heo hui-yeong, alihusianisha uwekezaji huo unaofanywa na serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan na sekta nyingine kama za utalii. Akionyesha kuvutiwa na ubunifu wa rais Samia, mh Heo aliongeza kuwa kwa karne hii ya 21 kuwa na vivutio peke yake kama mbuga za Wanyama, mito, maziwa, milima na fukwe za kuvutia sio kigezo pekee cha kupata watalii. Amempongeza rais Samia kwa kubuni namna za kuwarahisishia usafiri wa kufika Tanzania na kurudi makwao kwa kuwekeza kwenye shirika la ndege la Tanzania.
Katka hotuba yake hiyo, Mh. Heo Hui-yeong ameitabiria makubwa sekta ya anga ya Tanzania chini ya uongozi wa Dkt. Samia, akimtaja kama mwana mapinduzi mwenye mikakati ya kisasa na uelewa mkubwa wa masuala ya anga. Aliongeza pia chuo chao kipo tayari kuongeza ushirikano wa kimkakati na serikali ya Tanzania chini ya Mh. Dkt. Samia Suluhu. Ameitaja ziara hiyo ya Dkt. Samia Suluhu Hassan kama mwanzo wa uhusiano mrefu kati ya serikali ya Tanzania na chuo chao katika jitihada za kuiongezea tija sekta ya anga ya Tanzania.
Shahada hiyo imetolewa kama sehemu ya kumtia moyo Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuendeleza maboresho ya sekta mbalimbali za kimaendeleo kama njia ya kuinua uchumi wa Tanzania.